Friday, November 28, 2014

Bidhaa kutoka nje zawatesa wakulima

Arusha
Serikali imeshauriwa kutazama upya utaratibu wa kutoa vibali vya kuingiza nchini bidhaa mbalimbali kutoka nje ikiwamo sukari, ili kuwasaidia wakulima kupata soko la mazao wanayozalisha.

Mwenyekiti wa Umoja wa Taasisi ya Fedha Tanzania (TBA), Dk Charles Kimei alitoa wito huo hivi karibuni katika mkutano wa 17 wa TBA unaoendelea kufanyika jijini Arusha unaojadili changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya kilimo.

Dk Kimei alisema kuingizwa nchini kwa bidhaa kama sukari, kumesababisha viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo kushindwa kupata soko la uhakika la ndani na wakulima wanaolima miwa kwa ajili ya uzalishaji  wa sukari kushindwa kuuza zao hilo kwa wakati.

“Suala hili siyo tu linawaathiri wakulima bali pia linaathiri taasisi za fedha ambazo zinasaidia sekta ya kilimo,” alisema Kimei.


Katika hatua nyingine, Kimei alitoa wito kwa serikali kuunda bodi mbalimbali za mazao zitakazokuwa na jukumu la kuwatafutia masoko ya mazao wanayozalisha wakulima nchini.

No comments: