Monday, November 10, 2014

Airtel yazindua mpango kukopesha wafanyabiashara



Na mwandishi wetu

Kampuni ya Mawasiliano ya simu ya mkononi ya Airtel Tanzania, imezindua programu itakayowawezesha wafanyabiashara wadogo wadogo kukopa kirahisi fedha kupitia Airtel money.

Huduma hiyo ambayo inatolewa kwa kushirikiana na Kampuni ya AFB, imelenga kubadilisha maisha ya wafanya biashara wadogo ambao wanahitaji mikopo ili kuimarisha mitaji yao.

Huduma hiyo itajulikana kama”Airtel Timiza “ ni sehemu ya juhudi za Airtel kuungana na serikali katika kuwezesha wananchi na wateja wa Airtel wote kujipatia mikopo ya haraka na ya muda mfupi kwa marejesho nafuu ya siku 7 hadi 28 .

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Waziri wa Sayansi Teknolojia na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipongeza huduma hiyo na kusema ni motisha kwa wafanyabiashara wadogo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Sunil Colaso, alisema “leo uzinduzi wa huduma yetu ya Airtel money Timiza, unadhihirisha dhamira ya dhati ya Airtel ya kutoa huduma iliyo bora na nafuu ili kugusa maisha ya kila siku ya wateja wetu hapa Tanzania. “

Alisema ni matumaini yake kwamba huduma hiyo itaongeza kasi ya ukuzaji Uchumi miongoni mwa makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na vikundi vya wanawake, wajasiriamali na watu binafsi.

Kwa upande wake Mwanzilishi wa AFB, Andrew Watkins-Ball, alisema huduma hiyo ya mikopo ya Airtel money Timiza ni ya kipekee tofauti na benki ambayo ni lazima mteja kuwa na historia ya uwekaji na utoaji katika benki hiyo.


No comments: