Manyara
Wananchi wa wilaya ya Hanang’ wametakiwa
kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kwani utawawezesha kumiliki huduma za
afya, kutoa mawazo ya kuboresha huduma hizo na kuboresha huduma za matibabu
kupitia utaratibu rahisi na nafuu wa uchangiaji kwenye mifuko ya bima ya jamii.
Akiongea na waandishi wa habari jana, Meneja
wa NHIF mkoa wa Manyara, Innocent Mauki alisema matumizi ya fedha za CHF
yatanunua dawa, vifaa tiba, uboreshaji wa miundo mbinu ya afya na kutoa ajira
ya muda kwa wataalam wa afya.
Mauki, alifafanua kwamba wako baadhi ya
wananchi wilayani humo, wamekuwa wakilalamikia huduma za ukosefu wa madawa
hospitalini, lakini wanasahau kuwa sababu moja wapo ya upungufu huo ni kutotoa
michango ya kujiunga na CHF ili madawa yaweze kununuliwa kwa wingi.
Alisema maeneo yenye vituo vya afya na zahanati
yamekuwa na mwamko mkubwa wa wananchi wa
kujiunga na CHF kwa kuwa huduma za afya zimekuwa zikipatikana kwa urahisi,
tafauti na maeneo yasiyo na huduma hizo.
Alisema katika kuhamasisha watu kujiunga na
mfuko huo changamoto kubwa ni kuwaomba watu kwa hiari kujiunga na mfuko kwa
faida ya afya zao, badala ya huduma hiyo kuwa ya lazima kisheria.
“Sheria ya mfuko wa hiari kama CHF ingekuwa
ya lazima kwa kila kaya kujiunga, utekelezaji wake ungekuwa rahisi, badala ya
kuomba kaya hizo kujiunga kwa hiari, lakini tuna imani sheria hizo
zitarekebishwa mpango huu utawafikia watu wengi na kukubalika “ alisema Mauki.
No comments:
Post a Comment