Thursday, November 13, 2014

Ajali ya basi yaua wanne, wengine 40 wajeruhiwa



Na Mwandishi wetu

Basi la Wibonela ambalo hufanya safari zake kati ya kahama na Dar es Salaam limepinduka jana asubuhi na kuua watu wanne, akiwamo kichanga wa miezi mitatu, na kujeruhi wengine 40.

Katika ajali hiyo iliyotokea Kahama, mtu mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika, aliuawa kwa kupigwa na kisha kuchomwa moto na wananchi waliombaini wakati akitaka kuiba kompyuta ya mpakato kutoka kwa majeruhi.

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama, Joseph Ngowi alikiri kupokea majeruhi hao na kuongeza kuwa hali za watu wanne kati ya majeruhi hao ni mbaya wanaandaa utaratibu wa kuwapeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando Mwanza.

Ngowi aliwataja waliokufa kuwa ni kichanga Robinick Jordan, aliyekuwa na miezi mitatu na ambaye wazazi wake wote wawili wamejeruhiwa na kulazwa katika hospitali hiyo.

Ngowi aliwataja wengine waliofariki na miili yao kuhifadhiwa hospitalini kuwa ni Amina mkazi wa kigoma na Salum ambaye makazi yake hayakuweza kujulikana pamoja na mtu mmoja ambaye pia jina lake halikuweza kupatikana.

Alisema waliweza kupata jina mojamoja la majeruhi hao wawili.

Pia Ngowi alisema majina ya majeruhi 40 yanapatikana katika Hospitali hiyo ya Kahama.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Jastusi Kamugisha aliyefika eneo la tukio hilo, alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi.

Alisema dereva wa basi hilo alikuwa katika mwendo wa kasi na baadaye gari kumshinda na kusababisha ajali hiyo.

No comments: