Friday, November 14, 2014

Serikali yaonya wawekezaji feki

Dar es Salaam
Serikali imeyaonya baadhi ya Kampuni yenye nia ya kuja nchini kwa ajili ya uwekezaji katika sekta ya nishati, kuhakikisha hayashabikii vitendo vya rushwa.

Kampuni hizo zimetakiwa kabla ya kuja nchini, kujihakikisha hazina matatizo wala hazishabikii vitendo hivyo, kwani serikali imechoshwa na makampuni ya ubabaishaji na kwa sasa hayana nafasi tena.

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo katika mkutano uliowakutanisha wawekezaji zaidi ya 170 kutoka nchi mbalimbali duniani, uliofanyika Dar es Salaam.

Aidha, aliwataka Watanzania kutokubali kupotoshwa juu ya uwekezaji, kwani hakuna uchumi wa nchi yoyote duniani usiohusisha uwekezaji.

Alisema uwekezaji siyo dhambi na mtu anayefanya upotoshaji kuhusu uwekezaji hana nia njema, kwani anataka Waatnzania waendelee kuwa maskini.


Aidha, Muhongo alisema Mfuko wa Maendeleo wa Milenia(MCC) na Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji(EWURA) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) watatiliana saini kwa ajili ya kupewa fedha za kuanza miradi mikubwa.

No comments: