Monday, November 17, 2014

Gama ahimiza ujenzi wa vitega uchumi

Moshi
Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Leonidas Gama amesema maendeleo ya ujenzi wa Mji wa Moshi ili uwe wa kisasa utafanywa na wadau wenyewe ambao ni wakazi wa ndani na nje ya mji huo kwa lengo la kuleta maendeleo hasa ya kiuchumi.

Gama alisema yeyote mwenye nia hiyo ajitokeze na ofisi yake itamsaidia kupata ardhi haraka iwezekanavyo na amelisifu Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kuonyesha mfano kwa kuanza kujenga jengo moja la kisasa la kitega uchumi mjini hapa.

Akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo hilo lililoko Barabara ya Aga Khan, alisema litaongeza hamasa na kukuza soko la kimataifa kwa nchi za Tanzania na Kenya.

“Nayaomba mashirika, taasisi za kiserekali na binafsi mjitokeze kujenga majengo ya kisasa ya uwekezaji katika mji wetu ili tuongeze uchumi na hadhi ya mji huu, ofisi yangu haitasita kutoa ardhi kwa yeyote atakayejitokeza ili mradi tu afuate sheria, kanuni na utaratibu,” alisema Gama.


Alisema kupitia vikao vya RCC, wanakusudia kuiomba Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), kuupandisha hadhi Mji wa Moshi uwe jiji, baada ya kutimiza vigezo.

No comments: