Tuesday, November 25, 2014

Mwanga wamshukuru Prof. Maghembe, serikali kwa mabati

Waziri wa Maji ambae pia ni mbunge wa jimbo la Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe (katikati) akitoa maelekezo kwa baadhi ya watendaji wa vijiji vilivyoathirika na mafuriko yaliyotokea mwanzoni mwa mwaka 2013 Wilayani Mwanga mkoani Kilimanjro wakati wa zoezi la kugawa mabati kwa wathirika hao.  kushoto ni mratibu wa maafa wilaya ya Mwanga, Kiluvia Mzighani na kulia ni mmoja wa wazee walioathirika na mafuriko hayo Elia Msuya.
 
Waziri wa Maji ambae pia ni mbunge wa jimbo la Mwanga, Profesa Jumanne Maghembe (wa tatu kushoto) akimkabidhi mabati Bi. Evalista Yese (wa pili kulia) kutoka katika kijiji cha Mwaniko kata ya mwaniko wilayani mwanga mkoani Kilimanjaro hivi karibuni ambae ni mmoja wa waathirika wa mafuriko yaliyotokea mwanzoni mwa mwaka 2013 wilayani humo.  Kushoto ni mkuu wa wilaya ya Mwanga, Shwaiba Ndemanga.
Na Mwandishi Wetu, Mwanga

Wananchi waishio katika vijiji vya Vungi, Ubani, Vuchama Ngofi, Mriti na Mwaniko katika kata za Mwaniko na Kifula wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, wameishukuru serikali kwa msaada wa mabati.

Msaada huo wa mabati ulitolewa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mwanzoni mwa mwaka 2013 na kusababisha kaya zaidi ya 796 kukosa mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko.

Mabati hayo zaidi ya 2300 yametolewa na mbunge huyo, serikali pamoja na wadau wengine waliochangia.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti hivi karibuni mara baada ya kukabidhiwa mabati na mbunge wa Mwanga ambaye pia ni waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe,  wananchi hao walisema kuwa wamepata faraja kubwa baada ya kuona kilio chao kimesikika.

“Tunashukuru kwa hili, tulikua tunalala kwa majirani na mara nyingine hata nje,” alisema Gadi Msuya kutoka kijiji cha Vuchama Ngofi.

Naye Evalista Yese kutoka katika kikiji cha Mwaniko, alisema serikali imefanya jambo kubwa sana, huku akimshukuru mbunge wa jimbo hilo kwa juhudi kubwa aliyoifanya katika kutekeleza ahadi aliyowapa ya kuwapelekea mabati.

“Kati ya vitu vikubwa alivyofanya mbunge wetu katika kipindi hiki kigumu ni hili la kuleta mabati kwa wana Mwaniko,” alisema Evalista.


No comments: