Wednesday, November 5, 2014

Uda yaahidi huduma bora kwa abiria

Na Mwandishi wetu, Dar es Saalam

Wakazi wa Dar es Salaam wamekabidhishwa kupata huduma zilizoboreshwa zaidi kila watakapotumia mabasi yanayomilikiwa na Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), kutokana na mafunzo ya mwezi mmoja yanayotolewa na shirika kwa madereva, makondakta na wafanyakazi wengine wa shirika hilo.

Akizungumza wakati wa ziara ya waandishi wa habari katika makao makuu ya UDA jana, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na UDA, George Maziku alisema miongoni mwa mambo mengine, kampuni yake imejikita katika utoaji wa mafunzo madhubuti kwa wafanyakazi wake ili kuboresha huduma zote zinazotolewa kwa wateja.

Aliahidi uboreshaji wa huduma ikiwa pamoja na kuwajali wateja, suala ambalo limekuwa likizua mjadala mkubwa.

Maziku alisema kuwa kampuni yake ina mabasi yapatayo 400, jambo linaloifanya kuwa kampuni ya kwanza nchini kuwa na magari mengi yanayofanya kazi kwa mkupuo.

Alisema upo uhitaji mkubwa wa kuweka viwango thabiti, ambavyo vinaweza kuigwa na kampuni nyingine.


“Tunalenga kuwa na mabasi 3000 ifikapo mwakani, lakini kikubwa zaidi kabla hata ya kupata idadi hiyo ya mabasi ni kuwapa mafunzo madereva wetu ili wawe na elimu ya kutosha na uzoefu wa kutosha katika sekta ya usafirishaji wa umma,” alisema.

No comments: