Na Mwandishi wetu, Morogoro
Changamoto imetolewa kwa wasomi nchini kutumia taaluma
zao kubuni njia zitakazoleta suluhisho la matatizo na changamoto mbalimbali za
wananchi na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa mujibu wa naibu makamu mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Utawala
na Fedha, Profesa Faustin Kamuzora, ni kwa kuchukua hatua madhubuti za kutumia
taaluma zao kusaidia jamii ndipo wasomi hao watakuwa wamemuenzi hayati baba wa
Taifa kama inavyotakiwa.
Alikuwa akiongea hivi karibuni wakati wa Kongamano la
siku ya kumuenzi hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere liloandaliwa na chuo
hicho mjini Morogoro.
“Taaluma zetu zitumike kutafuta majawabu ya sera na
uvumbuzi wa aina mbalimbali ambao utasaidia kuleta mapinduzi ya kiuchumi,
kijamii na kitamaduni,”alisema.
Alisema watu wengi wamekuwa wakijipambanua kwa usomi wao
lakini hawakumbuki kuwa wana deni kwa jamii la kuwaletea majawabu ya matatizo
yao kupitia taaluma hizo.
“Kazi zetu zituonyeshe kuwa sisi ni wasomi,”alisema.
Alisema hakuna faida ya kujiita msomi wakati hakuna
jambo hata moja la kitaaluma ambalo mtu amelifanya kwa ajili ya taifa.
Alisema wakati nchi inapomkumbuka baba wa taifa, ni vyema
wasomi wakaiga mfano wake, kwani aliweza kuonyesha mfano kwa vitendo, kuongoza nchi
kwa uadilifu uliotukuka na kuandika vitabu mbalimbali.
“Tuige mfano wa baba wa taifa kwa kutenda na kazi zetu
zionekane na kuleta faida kwa jamii zetu na taifa kwa ujumla,” alisema.
No comments:
Post a Comment