Dar es Salaam
Ilikuwa hekaheka iliyosababisha
shughuli katika mitaa mine ya Tabata, Dar es Salaam kusimama kwa saa nne baada
ya kundi la vijana wenye nondo, mawe, visu kushambulia watu, kupora na kuharibu
mali kutokana na kile kilichodhaniwa kuwa ni kulipiza kisasi.
Kundi hilo la vijana zaidi ya 30
ambalo mmoja wao ameuawa linalofananishwa na Panya Road ambalo hivi karibuni
lilisimumbua jijini Dar es Salaam, liliamua kufanya vurugu hizo Jumamosi na
Jumapili baada ya ugomvi kutokea baina ya makundi mawili tofauti.
Makundi yaliyohusishwa na ugomvi huo
moja ni la Tabata Kimanga, Mtaa wa Magengeni na jingine ni la Tabata Kisiwani,
Mtaa wa Twiga.
Chanzo cha vurugu hizo zinaelezwa
kuwa ni kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Alfa Mhanga, Mkazi wa Tabata
Kisiwani kupigwa na kunyang’anywa simu na wenzake wa kundi jingine.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa
Mtendaji wa Kata ya Kisiwani, Herbert Haule alisema vijana hao waliingia
mitaani na kujeruhi watu, kuiba na kuharibu mali walipokuwa wakilipiza kisasi
baada ya mwenzao kupigwa.
Hata hivyo, Mkazi wa Kisiwani, Mwita
Mnofu alisema sakata zima la mkasa huo lilianza Jumamosi waakti vijana wawili
waliokuwa wakiangalia mpira kuzozana hadi kupigana na mmoja wa vijana hao
kwenda kutoa taarifa kwa kundi lake ambalo lilikuja kulipa kisasi.
“Unajua mmoja wa wale vijana
alipopigwa alikwenda kuwaita watu wa kundi lake ambao walikuja na kuanza
kuwatafuta wa kundi jingine na kuanza fujo ambazo ziliendelea hadi wakaanza kulipa
kisasi kwa watu wa mtaani kwa kuwapiga,” alisema.
Mama wa kijana mmoja aliyekuwa
anatafutwa na vijana hao, Hadija Mhenga alisema: “ Vijana zaidi ya 30 wakiwa na
mapanga, visu na marungu walikuwa hapa saa sita usiku na kuanza kupiga kelele
huku wakitaka kuchoma nyumba moto,” alisema .
Kijana mwengine, kinyozi katika
saluni iliyopo Uwanja wa Twiga, Gerald Manase alisema kundi la vijana kutoka
Tabata Kisiwani liliwakodi vijana wa Mabibo na kigogo kuja kulipa kisasi kwa
kupiga watu na kuwataka mapanga.
No comments:
Post a Comment