Dodoma
Serikali imesema itaendelea
kuwachukulia hatua kali za kisheria na za kinidhamu madaktari wote
watakaogundulika kujihusisha na utoaji wa mimba kinyume na utaratibu.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na
Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), Aggrey Mwanri alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Dimani, Abdallah
Sharia Amer kwa niaba ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii.
Mbunge huyo alitaka kujua serikali
inasema nini kuhusu suala la madaktari kuwatoa mimba wanafunzi.
Pia, alitaka kujua kama Serikali
inalitambua suala hilo,imechukua hatua gani za makusudi kukabiliana nalo.
Akijibu swali hilo, Mwanri alisema
utoaji mimba ni kosa la jinai ambalo linasimamiwa na Sheria ya Kanuni ya Adhabu
namba 16.
Aidha, alisema kitendo cha daktari
kufanya utoaji wa mimba ni kinyume na maadili ya taaluma ya uganga.
Alisema daktari au mtaalamu wa afya
endapo atapatikana na kosa kutoa mimba huchukuliwa hatua za kinidhamu bila
kujali cheo cha daktari husika.
“Suala la kumtoa mimba mama mjamzito
linaweza kufanyika tu pale ambapo itathibitishwa na jopo la madaktari kuwa
kuendelea kwa mimba hiyo kutahatarisha maisha ya mama,” alisema
Alisema hatua mbalimbali
zimechukuliwa na Serikali ili kukabiliana na tatizo la utoaji wa mimba ikiwamo
kuwakumbusha mara kwa mara viongozi wa hospitali zote na vituo vya huduma za
afya nchini kusimamia kanuni za utumishi wa umma na maadili ya kitaaluma.
No comments:
Post a Comment