Na Mwandishi wetu, Dodoma
Matumizi sahihi ya teknolojia ya
kisasa yametajwa kama nyenzo muhimu itakayosaidia kuendelea kutoa huduma bora
za maji kwa wakazi wa mijini na vijijini hapa nchini.
Kwa sababu hiyo, serikali imesema
suala la kujenga uwezo wa raslimali watu na vifaa mbalimbali vya kusimamia
mifumo ya maji kwa kuzingatia teknolojia mpya lina umuhimu wa kipekee ili
kufikia malengo ya huduma za maji kwa kasi zaidi.
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe
amesema hayo wakati wa mkutano wa 15 wa mwaka wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa
Mazingira Mijini hivi karibuni mjini Dodoma.
”Teknolojia inabadilika kila
kukicha na uendelezaji wa huduma ya maji unahitaji kwenda sambamba na
mabadiliko hayo,” alisema Waziri Maghembe.
Akitoa mfano, alisema Mamlaka
zitumie teknolojia (ICT) katika utoaji huduma, ukusanyaji wa takwimu,
utayarishaji wa ankara na malipo na vifaa vya kujua upotevu wa maji, ili
kuendana na mabadiliko ya ukuaji wa teknolojia.
Mada kuu ya Mkutano huo
ilikuwa “Usimamizi wa
Miundombinu ya Maji kwa Uendelevu wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira
Nchini”
Pamoja na changamoto zilizopo,
Prof. Maghembe alizipongeza Mamlaka za Mikoa kwa jukumu kubwa la kutekeleza
lengo la kuwapatia Watanzania huduma ya maji safi na salama.
No comments:
Post a Comment