Wednesday, November 12, 2014

Mtoto aliyepotea auawa kikatili, maiti yaokotwa

Dar es Salaam
Mtoto Nuru Mohamedi (7) ameuawa kikatili na kisha mwili wake kutelekezwa kwenye nyumba ambayo haijakamilika ujenzi iliyo Majohe Kichangani mjini hapa.

Tukio hilo, ambalo limezua hofu na huzuni kwa wakazi wa mtaa huo, lilibainika jana baada ya kupatikana kwa maiti ya huyo ambaye kabla ya umauti kumkuta alikuwa amepotea katika mazingira ya kutatanisha tangu Novemba 6.

Akisimulia tukio hilo kwa tabu huku akilia kwa huzuni, mama mzazi wa mtoto huyo, Sauda Ally alisema Alihamisi iliyopita saa 1:00 usiku mtoto wake alikuwa akicheza nje ya nyumba yao pamoja na watoto wengine wawili.

“Baadaye akaja mtoto wa jirani aitwaye Dula, akaniambia Nuru amekwenda na babu mmoja alimwambia amsindikize dukani, nilinyanyuka haraka na kutoka nje na kuanza kumwita, lakini hakuitika,” alisema.

Alisema baada ya kuona hali hiyo alikimbia hadi dukani alikoelekezwa kuwa mwanaye amekwenda, lakini hakumwona hivyo aliamua kuomba msaada kwa majirani na taarifa zilipelekwa katika msikiti wa karibu kwa ajili ya kutangazwa na kisha waliendelea kutoa taarifa hizo kituo cha polisi cha Gongo la Mboto.

Alisema mtoto wake alitafutwa bila mafanikio kwa siku sita.

Alisema jana asubuhi mmoja wa wapangaji wake alipokea simu kutoka kwa jirani yake anayeishi eneo la kwa Mkandawile kwamba kuna maiti ya mtoto imeonekana katika maeneo hayo na kwamba huenda akawa ni mtoto wake.


Hata hivyo Sauda alishindwa kuelezea zaidi mkasa huo na mama mkubwa wa marehemu, Rehema Ally alisema kuwa baada ya simu hiyo waliondoka mara moja kwenda eneo la tukio.

No comments: