Wednesday, November 5, 2014

Mtoto achanwachanwa kwa wembe

Morogoro

Mkazi wa Mtaa wa Kiwalani, Manispaa ya Morogoro, Jafari Mashaka (11) amechanwachanwa na wembemiguuni, mikononi kasha kupigwa na mwanamke anayedaiwa kuwa ni mama yake mdogo kwa kumtuhumu kuiba Sh4,500.

Tukio hilo linadaiwa kufanywa Novemba Mosi, mchana na mwanamke huyo Tausi Omary (30) anayeishi na Jafari.

Akizungumza baada ya kufikishwa katika dawati la jinsia la Polisi na wasamaria wema, Jafari alidai kuwa mama yake mdogo alikuwa akimpiga kila siku na kumnyima chakula.

Tausi alipohojiwa alikiri kumfanyia ukatili huo motto, huku akijitetea kuwa shetani alimpitia anaomba asamehewe.

“Ni kweli nimefanya tukio hili, lakini nia yangu ilikuwa ni kumwonya,Jafari ana tabia ya wizi, kila mara huwa ananiibia fedha ndani na kwenda kucheza pool table na nyingine anakwenda kununua mihogo,” alisema.

Mama mzazi wa motto huyo alisema: “Nimerudi usiku kutoka kwenye biashara zangu nikaambiwa na majirani kuwa Jafari kakatwa viwembe na mama yake mdogo, lakini sikujua kama alimjeruhi kwa kiwango kikubwa hivi.”

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kiwalani, Salvatory Lipende alisema alitoa taarifa polisi baada ya kusikia ukatili alioufanyiwa Jafari kutoka kwa majirani.


Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto, Inspekta Msaidizi wa Polisi, Sophina Ngoso alisema matukio ya ukatili hasa kwa watoto yamekuwa yakiibuliwa kila siku.

No comments: