Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) imetakiwa kuharakisha mchakato wa kupata sheria itakayosaidia Wakala wa Mradi wa Mbasi Yaendayo
Haraka (DART) kupata sehemu ya kodi ya mafuta ili zisaidie ukarabati miundombinu
yake.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge TAMISEMI, Dk. Hamisi
Kigwangala aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kuwa sheria hiyo
ikiwa tayari itasaidia wakala huo kuwa na nguvu za kifedha kusaidia katika
shughuli za ukarabati wa miundombinu yake.
“Mradi huu ni wetu sisi sote hivyo ni jambo jema kukawa
na sheria kama hii ya kupata fedha toka
kodi ya mafuta,”alisema jijini Dar es Salaam baada ya kikao kati ya kamati yake
na uongozi wa wakala wa DART.
Alisema miundombinu hiyo imejengwa kwa gharama kubwa na
ni lazima pawe na utaratibu wa kuifanyia ukarabati kwa wakati unaotakiwa ili
iweze kuwa endelevu na kutoa huduma bora.
Pia alielezea haja ya serikali kuwa mkakati endelevu wa
miradi ya barabara, reli, barabara za juu katika maeneo yote ya nchi yanayokua
kwa haraka.
Alisema kwa sasa serikali inaingia gharama kubwa ya
kulipa fidia wananchi maeneo yao kupisha miradi kama hiyo kwa sababu hakuna
mikakati endelevu na mipango ya muda mrefu.
“Ni vyema jambo hili likafanyika mapema katika
halmashauri zetu na majiji ili kuokoa gharama siku za baadaye,” alisema.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa DART, Bi, Asteria
Mlambo alisema wakala umeshapeleka maombi maalumu Wizara ya Ujenzi ili kupatiwa
fedha za matengenezo ya barabara za mradi zitokanazo na makusanyo ya kodi ya
mafuta.
No comments:
Post a Comment