Monday, November 10, 2014

Kikwete afanyiwa upasuaji Marekani



Dar es Salaam

Rais Jakaya Kikwete amefanyiwa upasuaji wa tezi dume (Prostate) katika Hospitali ya Johns Hopkins iliyoko Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani.

Taarifa iliyotoplewa na Mkurugenziwa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salva Rweyemamu kwa vyombo vya habari jana imesema Rais Kikwete amefanyiwa upasuaji huo juzi alfajiri baada ya madaktari waliomfanyia uchunguzi wa afya yake kujiridhisha kuwa alikuwa anahitaji matibabu ya aina hiyo.

“Upasuaji huo ulifanyika alfajiri na kuchukua kiasi cha saa moja unusu, umefanyika salama na kwa mafanikio makubwa,” ilisema taarifa hiyo na kubainisha kuwa hali ya Rais Kikwete inaendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari na kupatiwa tiba.

Taarifa hiyo iliyoambatana na picha mbili moja ikimwonyesha Rais Kikwete akiwa anazungumza na daktari bingwa wa upasuaji katika hospitali hiyo, Dk Edward na nyingine akiwa ameketi pamoja na daktari huyo na daktari wake, Profesa Mohamed Jabil alisema wananchi wataendelea kupewa taarifa sahihi kuhusu hali ya Rais kwa kadri zitakavyokuwa zinapatikana.

Wiki iliyopita, Kurugenzi hiyo ya mawasiliano Ikulu ilitoa taarifa za safari ya Rais Kikwete kwenda Marekani kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake na kuwa angekaa huko kwa siku 10.


No comments: