Thursday, December 4, 2014

Jumla ya wahitimu 3943 kutunukiwa Mzumbe kuanzia leo

Na Mwandishi wetu, Morogoro

Chuo Kikuu Mzumbe kinatarajia kuwatunuku jumla ya wahitimu 3943 katika madaraja mbalimbali kuanzia leo tarehe 5 Desemba.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chuo hicho, Bi. Rainfrida Ngatunga jana mahafali katika kampasi kuu yanafanyika leo ambapo jumla ya wahitimu 2125 watatunukiwa.

“Kati ya hao, wanawake ni 922 na wanaume ni 1174,” alisema Bi. Ngatunga katika taarifa hiyo.

Mahafali katika kampasi ya Mbeya yatafanyika wiki ijayo tarehe 12 ambapo 832 watatunukiwa.  Kati yao wanawake ni 444 na wanaume ni 388.

Shughuli za mahafali ya chuo hicho zitakamilika katika kampasi ya Dar es Salaam tarehe 19 mwezi huu ambapo wahitimu 986 watatunukiwa.  Kati ya hao wanawake ni 473 na wanaume ni 513.

Kwa mujibu wa Afisa huyo, wahitimu wa vituo vya kufundishia vya Mwanza na Tanga watahudhuria mahafali Kampasi Kuu. 

Mhitimu mmoja ambaye ni Mhadhiri wa chuo hicho, Bw. Joseph Sangau atatunukiwa shahada ya uzamivu PhD.


Mahafali hayo yote yatahudhuriwa na Mkuu wa chuo hicho, Jaji Mstaafu, Barnabas Samatta na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Josephat Itika, miongoni mwa viongozi wengine.

No comments: