Sunday, December 7, 2014

Vyuo vya Mzumbe, Tampere kuendesha utafiti kuimarisha maisha ya kaya nchini



Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Jaji Mstaafu Barnabas Samatta akimtunuku shahada ya uzamivu (Phd) mmoja wa wahitimu, Joseph Sangau, katika mahafali ya 13 ya chuo hicho yaliyofanyika katika kampasi kuu mjini Morogoro mwishoni mwa wiki.  Kushoto ni Kaimu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Josephat Itika.


 Sehemu ya wahitimu wa mahafali ya 13 ya chuo kikuu Mzumbe yaliyofanyika katika kampasi kuu ya chuo hicho mjini Morogoro mwishoni mwa wiki.


 Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Utawala na Fedha, Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Faustin Kamuzora (Kushoto) akijadili jambo na Rais wa Masajili wa Chuo hicho, Bw. Ludovic Utouh wakati wa mahafali ya 13 ya chuo hicho yaliyofanyika katika kampasi kuu mjini Morogoro mwishoni mwa wiki.


 
 Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Jaji Mstaafu Barnabas Samatta (katikati) wakati wa mahafali ya 13 ya chuo hicho yaliyofanyika katika kampasi kuu mjini Morogoro mwishoni mwa wiki.  Kulia ni Kaimu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Josephat Itika na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Prof. Daniel Mkude (kushoto).


Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Chuo Kikuu Mzumbe kimeanzisha ushirikiano na Chuo Kikuu cha Tampere cha nchini Finland kufanya utafiti utakaosaidia kujenga uwezo na hali bora ya maisha katika kaya nchini Tanzania.

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Josephat Itika amesema ushirikiano huo unalenga kuja na majibu ya kuboresha  hali ya maisha ya kaya katika Tanzania.
Alikuwa akizungumza wakati wa mahafali ya 13 ya chuo hicho mjini Morogoro mwishoni mwa wiki.

“Utafiti huu unalenga kuboresha hali ya maisha ya kaya kutokana na ukweli kwamba kuna tatizo la umasikini katika kaya zetu,”alisema.

Alisema utafiti huo utakuja na mbinu mpya itakayosaidia kuleta ufumbuzi juu ya swala la umasikini katika kaya ili kuondokana nao.

Inatarajiwa kwamba utakapokamilika, utafiti huo utapelekwa kwa wadau mbalimbali ikiwemo serikali ili hatua za makusudi ziweze kuchukuliwa.

Alifafanua kwamba kaya zikiwa na maisha mazuri, ni kiashiria kikubwa kwamba vipato vya jamii vimekua na kukua huko hujenga uchumi wa nchi.

Katika miaka ya hivi karibuni, Mzumbe imekuwa ikizidisha ushirikiano na vyuo vya nje ili kujijengea uwezo katika maeneo ya ufundishaji, utafiti na huduma za ushauri.

No comments: