Monday, December 22, 2014

Watanzania washauriwa kujenga tabia ya kununua hisa

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wito umetolewa kwa Watazania kujenga tabia ya kununua hisa katika kampuni ikiwemo ya kampuni Uwekezaji ya TCCIA kwa maendeleo yao na taifa zima kwa ujumla.

Wito huo ulitolewa na wakala wa uuzaji Hisa wa kampuni ya Rasilimali Limited, Bw. Arphaxad Masambu ambaye pia ni mjumbe wa kampui ya TCCIA alipokua akitoa semina kwa wanahisa wa kampuni hiyo hivi karibuni jijini humo.

Mtaalamu huyo alisema wakati umefika wa watanzania kuelewa maana ya hisa na kuanza kuzinunua.

“Tunatakiwa kubadilika kwa sababu swala hili limekuwa kama geni kwetu, sasa wakati umefika wa kuchukua hatua na kupenda kujifunza ili hisa zitusaidie baadaye,”alisema.

Akifafanua zaidi alisema kuwa na hisa katika kampuni ni ukombozi mkubwa katika maisha sababu fedha zinakuwa katika mazingira salama na zinaongezeka.

Alisema kampuni ya hisa kazi yake ni kukusanya mtaji ambao unatokana na hisa walizonunua watu na kwenda kuwekeza katika makampuni na mashirika yanayojiendesha kwa faida.


“Kampuni ya hisa inaendeshwa kwa mujibu wa sheria za nchi, hivyo watanzania wasisite kununua hisa katika kampuni zinazofanya vizuri,”alisema.

No comments: