Tuesday, January 13, 2015

Serikali yasifu ushirikiano wa kampuni ya Serengeti, wakulima

Meneja wa kiwanda cha bia cha kampuni ya Serengeti mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Bw. Gideon Kabuthi (kulia) akimuongoza Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Bi. Janet Mbene katika maeneo mbalimbali ya kiwanda hicho mwishoni mwa wiki mkoani humo.  Waziri huyo alitembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji katika kiwanda hicho pamoja na kufanya mazungumzo na uongozi na wafanyakazi wa kiwanda hicho.
Meneja wa kiwanda cha bia cha kampuni ya Serengeti mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Bw. Gideon Kabuthi (kulia) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Bi. Janet Mbene mwishoni mwa wiki mkoani humo.  Waziri huyo alitembelea maeneo mbalimbali ya uzalishaji katika kiwanda hicho pamoja na kufanya mazungumzo na uongozi na wafanyakazi wa kiwanda hicho.
Na Mwandishi wetu, Moshi

Serikali imesema mpango wa ushirikiano kati ya kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) na wakulima wadogo nchini unafaa kuigwa na wawekezaji wengine nchini Tanzania.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Bi. Janet Mbene amewaambia waandishi wa habari hivi karibuni mjini Moshi kuwa mpango wa kampuni hiyo ya bia wa kununua mazao kwa wakulima unasaidia kuboresha maisha ya wananchi kwa kiasi kikubwa.

Chini ya mpango huo, kampuni hiyo inawasaidia wakulima wa shayiri mbegu na kuwaunganisha na wataalamu wengine wa kilimo ambapo hatimae hununua zao hilo.

Waziri huyo alitembelea kiwanda hicho kilichoko Moshi mkoani Kilimanjaro kama moja ya ziara zake kutembelea viwanda katika kanda ya kaskazini.

SBL inatumia malighafi ya ndani kuzalisha baadhi ya bidhaa zake.  Inatumia kwa asilimia 100 ya malighafi hiyo ambayo ni mtama, mahindi na shayiri kutengenezea bia aina ya Kibo Gold, Uhuru Lager, the Kick, Pilsner na Senator.

“Hii ni namna bora kabisa ya kujenga mahusiano kati ya wawekezaji kwa upande mmoja na wakulima na wajasiriamali kwa upande mwingine...SBL imetupa mfano mzuri,” alisema na kuongeza kuwa mpango huo unawahakikishia soko la uhakika wakulima.


No comments: