Wednesday, January 21, 2015

DART yachukuliwa kupunguza msongamano kituo cha Ubungo



Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Hatua kadhaa zimechukuliwa kujaribu kurahisisha utokaji wa mabasi ya kwenda mikoani katika kituo cha mabasi cha Ubungo (UBT).

Hatua hizo, zilizokubaliwa jana na wakala wa mradi wa mabasi yaendayo haraka (DART),mshauri wa mradi wa DART, SMEC na mkandarasi wa mradi huo, STRABAG zinalenga kupunguza msongamano wa magari katika eneo hilo hasa nyakati za asubuhi, mabasi hayo yanapokuwa yanatoka kuelekea mikoani.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa miundombino na Uendeshaji wa wakala wa DART,Mhandisi John Shauri, ukingo unaotazamana na Geti namba 1 la Kituo cha Mabasi cha Ubungo (UBT) unaotenga barabara ya kawaida na njia ya mradi utabaki kama ulivyojengwa.

Mhandisi aliongeza kuwa mabasi ya mikoani yanayoondoka UBT kupitia Geti namba 1 au 2 yataruhusiwa kutumia njia za mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) zinazotazamana na Geti namba 2 na kisha kugeuza kwa kutumia njia hizo wanapofika katika kituo cha basi cha mradi cha BRT Ubungo na kuelekea katika mataa ya Ubungo yakitumia njia hizo hizo za mradi.

“Baada ya hapo watatumia barabara ya kawaida kuelekea Kimara,” ilisema na kuongeza kuongeza mabasi hayo yatatumia kwa muda kwenye njia hizo mpaka pale tu huduma za kipindi cha mpito (interim service) kwenye barabara za mfumo wa mabasi yaendayo haraka kitapoanza.

No comments: