Wednesday, January 21, 2015

Serengeti Ltd yawaahidi makubwa wakulima wa shayiri nchini



Na Mwandishi wetu, Siha

Kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) imesema kwamba wakulima katika kanda za kilimo cha shayiri Tanzania wategemee ushirikiano zaidi kupitia mpango wa kampuni hiyo kushirikiana na wakulima wadogo wa zao hilo nchini.

Akiongea na waandishi wa habari wilayani Siha mkoa wa Kilimanjaro hivi karibuni, Meneja Kilimo Biashara wa kampuni hiyo ya SBL, Bw. Shafii Mndeme alisema mkakati huo uko mbioni kuimarishwa katika miaka miwili ijayo na zaidi.

Kwa mujibu wa mpango huo, kampuni hiyo inawasaidia wakulima wa shayiri mbegu na kuwaunganisha na wataalamu wengine wa kilimo ambapo hatimae hununua zao hilo.

Kampuni hiyo pia inasaidia wakulima kupata elimu kuhakikisha kuwa mazao wanayozalisha yanakua ya kiwango bora kwa uzalishaji wa bia pamoja na kuongeza uzalishaji kwa heka.

“Wakulima wa shayiri nchini walime zao hilo maana mpango huu unazidi kukua siku hadi siku,” alisema mara baada ya kugawa mbegu za zao hilo kwa wakulima wa kijiji cha Ngare Nairobi wilayani Siha.

No comments: