Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Kampuni ya Uwekezaji ya TCCIA (TCCIA Investment Company Limited)
imewataka wanahisa wake kushiriki Mkutano Mkuu wa tisa wa mwaka kufanyika
kesho kwenye Ukumbi wa Karimjee ambao utatoa fursa ya kujionea maendeleo
yaliyofikiwa na kujadili maswala mbalimbali ya kampuni.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni hiyo, Bw. Donald Kamori, aliwaambia
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa mkutano huo ni muhimu sana
kwa wanahisa wote na hivyo ni vizuri wakashiriki na kupata fursa ya
kujua maendeleo ya kampuni.
“ Mkutano huo utatanguliwa na semina ambayo inalenga kutoa elimu zaidi
kwa wanahisa juu uwekezaji kwa njia ya hisa, faida na changamoto zake,”
alisisitiza Bw.Kamori na kutoa wito kwa wanahisa kushiriki kwa wingi.
Alisema baada ya semina hiyo mkutano mkuu utafunguliwa na Mwenyekiti wa
Bodi, Mhandisi Aloys Mwamanga kama ilivyo kawaida kwa mikutano
iliyotangulia tangu mwaka 2006.
Kwa mujibu wa Bw. Kamori, kufanyika kwa mkutano pia utakidhi
matakwa ya Sheria ya Msajili wa Makampuni (BRELA) ya mwaka 2002
ambayo inataka kila kampuni iliyosajiliwa kufanya mkutano kila mwaka.
Alisisitiza kuwa wanahisa wanahitajika kushiriki mkutano huo kwa vile
kampuni watawapa fursa ya kupokea, kujadili na kuridhia taarifa
mbalimbali zitakazowasilishwa mbele ya mkutano mkuu.
No comments:
Post a Comment