Wednesday, December 10, 2014

Wahadhiri wapewa changamoto ya kuzidi kufanya tafiti, ushauri



Na Mwandishi wetu, Morogoro
Wahadhiri wa chuo Kikuu Mzumbe wamepewa changamoto kuzidi kufanya tafiti, ushauri wa kitaalamu na kutoa machapisho mbalimbali ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya tasnia ya elimu na taifa kwa ujumla.

Changamoto hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Profesa Daniel Mkude wakati wa mahafali ya 13 ya chuo hicho hivi karibuni mjini Morogoro.

Prof. Mkude alisema jukumu la kazi hizo za tafiti na ushauri wa kitaalamu linaangukia mikononi mwa wahadhiri na hivyo hawana budi kuongeza bidii na kufanya kazi hiyo vizuri.

“Haya ni maeneo muhimu sana kwa maendeleo yenu binafsi, ya chuo na taifa kwa jumla...ni muhimu kuongeza bidii na weledi katika hili,” alisema.

Aliwapongeza wahadhiri walioshiriki kufanya tafiti, kuandika na kutoa machapisho yakiwemo ya vitabu, makala na ripoti mbalimbali katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Akifafanua zaidi alisema kazi  hizo za kitaaluma ndizo zinazosaidia chuo kukuza elimu na kuwa shindani, hivyo wahadhiri hawana budi kuendelea na kuongeza nguvu katika maeneo hayo.

No comments: