Monday, December 22, 2014

Wateja wa Zantel, Tigo kufaidika na huduma mpya ya kutuma, kupokea fedha

Mkurugenzi wa Huduma za Fedha Zantel, Bw. Hashim Mukudi (wa pili kushoto) akipongezana na Mkuu wa kitengo cha Huduma za Fedha wa kampuni ya Tigo, Bw. Andrew Hodgson  wakati wa uzinduzi rasmi wa huduma mpya ya kutuma na kupokea pesa miongoni mwa wateja wa mitandao hiyo hapa nchini jana visiwani Zanzibar.  Kulia ni Meneja Chapa wa Tigo, Bw. William Mpinga na kushoto ni Bi. Shinuna Kasim ambae ni Mkurugenzi wa Miradi wa Zantel.
Na Mwandishi wetu, Zanzibar

Kampuni za simu za mkononi za ZANTEL na Tigo zamezindua rasmi huduma za kutumiana pesa miongoni mwa wateja wake Tanzania.

Mbali na huduma hiyo ya kutumiana pesa miongoni mwa wateja wa mitandao hiyo, wateja wa EzyPesa na TigoPesa sasa wataweza kutuma na kupokea pesa kwa marafiki na ndugu walio katika mitandao hiyo popote pale nchini.

Kutekelezwa kwa mpango huo kunazifanya ZANTEL na Tigo kuwa viongozi wa huduma kama hiyo Duniani. 

Uzinduzi wa huduma hiyo umefanyika visiwani Zanzibar jana na kushuhudiwa na maafisa wa juu wa kamuni hizo.  Haya ni matokeo ya makubaliano yaliyotangazwa mwanzoni mwa mwaka huu na EzyPesa, TigoPesa na Airtel Money.  

Kwa mujibu wa maafisa hao, hapatakuwa na gharama za ziada mteja anapotuma pesa kwa mtandao mwingine isipokuwa gharama zinakuwa sawa na zile anapotuma kwenye mtandao wake.

Pia, wateja wanaopokea pesa kutoka mtandao mwingine wanaweza kutoa pesa kwa wakala wa mtandao wao na hapatakuwa tena na ulazima wa mteja kutafuta wakala wa mtandao wa mtu aliyemtumia pesa.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Biashara wa Zantel, Mohamed Mussa, alisema Zantel inaendelea kutimiza ahadi ya kuwarahisishia huduma za fedha wateja wake kwa kufanya kazi pamoja na Tigopesa.

No comments: