Arusha
Serikali imeshauriwa kutazama upya
utaratibu wa kutoa vibali vya kuingiza nchini bidhaa mbalimbali kutoka nje
ikiwamo sukari, ili kuwasaidia wakulima kupata soko la mazao wanayozalisha.
Mwenyekiti wa Umoja wa Taasisi ya
Fedha Tanzania (TBA), Dk Charles Kimei alitoa wito huo hivi karibuni katika
mkutano wa 17 wa TBA unaoendelea kufanyika jijini Arusha unaojadili changamoto
na fursa zilizopo katika sekta ya kilimo.
Dk Kimei alisema kuingizwa nchini kwa
bidhaa kama sukari, kumesababisha viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo kushindwa
kupata soko la uhakika la ndani na wakulima wanaolima miwa kwa ajili ya
uzalishaji wa sukari kushindwa kuuza zao
hilo kwa wakati.
“Suala hili siyo tu linawaathiri
wakulima bali pia linaathiri taasisi za fedha ambazo zinasaidia sekta ya
kilimo,” alisema Kimei.
Katika hatua nyingine, Kimei alitoa
wito kwa serikali kuunda bodi mbalimbali za mazao zitakazokuwa na jukumu la
kuwatafutia masoko ya mazao wanayozalisha wakulima nchini.