Wednesday, October 1, 2014

Watanzania washauriwa kutumia mfumo wa KAIZEN kuleta tija


Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Florens Turuka (katikati) akifuatilia jambo wakati wa mkutano wa Taasisi ya Maafisa Wakuu Watendaji (CEOs Round Table) katika semina kuhusu umuhimu wa kutumia utaratibu huo wa KAIZEN kuchochea maendeleo Jumanne jijini Dar es Salaam.  Kulia ni Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada na Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Viwanda, Bw. Uledi Musa.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Florens Turuka (wa pili kulia) akifurahia jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Prof. Samuel Wangwe (kulia) wakati wa mkutano wa Taasisi ya Maafisa Wakuu Watendaji (CEOs Round Table) katika semina kuhusu umuhimu wa kutumia utaratibu huo wa KAIZEN kuchochea maendeleo Jumanne jijini Dar es Salaam.  Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Viwanda, Bw. Uledi Musa na Muwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Japan (JICA) Tanzania, Bw. Yasunori Onishi (kushoto).
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Watanzania wameshauriwa kujifunza na kuutumia mfumo wa KAIZEN ambao unalenga  kuongeza tija katika utendaji kazi, kuleta ufanisi wa uzalishaji na ubora ili kuchochea maendeleo nchini.

Wito huo ulitolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Florence Turuka wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mara tu baada ya kufungua mkutano wa Taasisi ya Maafisa Wakuu Watendaji (CEOs Round Table) katika semina kuhusu umuhimu wa kutumia utaratibu huo wa KAIZEN kuchochea maendeleo.

“Utaratibu huu unalenga kuleta mabadiliko ya kifikra na ujuzi sehemu za kazi na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa na kampuni au taasisi zetu hapa nchini,”alisema Dk. Turuka aliyemuwakilisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
KAIZEN ni dhana iliyoanzia na kutumika nchini Japan na kuaminika kuleta mapinduzi makubwa ya maendeleo katika nchi hiyo ikilenga kufikiwa kwa mapinduzi ya viwanda.

Kimsingi, mfumo huo unalenga kuongeza thamani na uzalishaji kwa kuwawezesha wananchi mbinu bora za kazi na usimamizi katika maeneo yao ya kazi.

“Utaratibu huu ni wa mabadiliko ya fikra kwa wafanyakazi na waajiri wao sehemu za kazi na kutumia fursa hiyo kuwawezesha wafanyakazi kupata ujuzi zaidi na vitendea kazi bora kutoa huduma bora,”alisema.

Dk. Turuka alisema utaratibu huo haulengi tu sekta binafsi, bali pia sekta ya umma ambayo inatakiwa kushirikiana na sekta hiyo ili kufikia malengo ya nchi.

Balozi wa Japani nchini, Bw. Masaki Okanda alisema utaratibu huo ni wa kubadili fikra kwa kampuni au taasisi katika uendeshaji kwa nia  ya kuleta tija na ubora wa uzalishaji.

“Japani imefanikiwa sana katika utendaji na ubora huduma kupitia utaratibu huu wa KAIZEN na mnaweza kuutumia mpate mafanikio,” alisema.

Alisema Tanzania ina rasilimali nyingi na kuna kampuni na taasisi nyingi lakini inatakiwa kuimarisha utaratibu wa kujenga ujuzi kwa ajili ya kuongeza tija na ubora wa huduma.

Alisema panahitajika kuwawezesha wafanyakazi sehemu za kazi na kuweza kuleta mabadiliko ya uzalishaji bora na kuwa kichocho katika kuleta mabadiliko ya maendeleo.

Naye, Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Japan (JICA) Tanzania, Bw. Yasunori Onishi aliipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara na Tanzania KAIZEN Unit katika jitihada inazozifanya kwa kushirikiana na shirika lao katika kuimarisha swala hilo.

Alisema utaratibu huo uliasisiwa Japan na kuwapatia mafanikio makubwa ambao  unalenga zaidi ushirikishwaji wa watu wa chini.

Mfumo huo sasa unatumika kama njia ya kuleta mabadiliko na tayari mataifa mbalimbali duniani wanautumia zikiwemo nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kama Ghana, Kenya na Zambia.

Mhandishi wa Kampuni ya TAPCO, Shabbier Khataw ambae kampuni yake inatumia mfumo huo alisema umewaletea mafanikio makubwa katika utendaji, uzalishaji na ubora wa huduma wanazotoa.

Hadi sasa kuna kampuni 32 Tanzania ambazo zinatumia mfumo huu kwa majaribio.

“Utaratibu huu ni muhimu kama tunataka kuendelea katika sekta ya viwanda...ni viwanda pekee ndivyo vitalikwamua taifa hili,”alisema.

Mkutano huo wa majadiliano uliandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara, Tanzania KAIZEN Unit Kwa kushirikiana na Shirika la kimataifa la Japani la JICA.


Mwisho

No comments: