Wednesday, October 29, 2014

Shirika la Posta lajiimarisha kidigitali

Dar es Salaam
Shirika la Posta Tanzania (TPC) limeanzisha mradi wa utekelezaji ili kuziwezesha ofisi za posta nchini kuunganishwa katika mfumo wa kielekitroniki ujulikanao kama “Post Global.”

Mradi huo ni hatua za shirika hilo kutoa huduma za kisasa zinazokwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Pia mwelekeo wa shirika hilo ni kuanza kutoa uwakala wa huduma za serikali mtandao katika vituo vyote kwa lengo la kupunguza gharama na kero kwa wananchi .

Meneja mkuu uendeshaji biashara wa shirika hilo, Fortunatus Kapinga, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa hatua hiyo imetokana na dhamira ya ushirika kusambaza matumizi ya teknolojia kwa wananchi wa vijijini na mjini.

Kapinga alisema hivi sasa, ofisi 97 zimeonganishwa huku wakitarajia ifikapo mwishoni mwa mwaka huu kuwa na zaidi ya ofisi 100 zilizo unganishwa na mfumo huo.

Pia alisema shirika limeanzisha mafunzo kupitia njia ya mitandao kwenye vituo vya mawasiliano ya jamii katika ofisi za Zanzibar, Arusha, Bagamoyo, Mwanza na Mbeya. Lengo la kufanya elimu ya mtandao kwa wananchi katika kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii.


No comments: