Na mwandishi wetu, Kibaha
Mkuu wa mkoa wa Pwani,Mwantumu Mahiza amesema umaskini siyo
sifa wala ulemavu,hivyo kila mwananchi anapaswa kutumia fursa ndogo anayoipata
ili kuondokana na hali hiyo.
Akizungumza mjini hapa hivi karibuni, alisema endapo wananchi
watatumia kwa umakini mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (Tasaf),umaskini unaweza kuwa historia.
Alisema katika utekelezaji wa mpango huo, kuna haja ya
kuangalia eneo jingine la wasusi ambao wakipewa mitaji na vikapu vitakavyokuwa
mbadala wa mifuko ya plastiki inayochafua mazingira.Mahiza aliwataka
watakaosimamia mpango huo kujizatiti kiutendaji na kuhakikisha kuwa malengo
yake yanafanikiwa.
Pia alisisitiza kwamba uteuzi wa walengwa waliokusudiwa
ufanyike kwa kufuata miongozo na taratibu zilizowekwa ikiwamo kushirikisha
jamii bila upendeleo.
Awali,akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi mtendeji wa Tasaf,
Mkuu Kitengo cha mawasiliano wa mfuko huo, Zuhura Mdungi alisema mpango huo unatarajia
kuzifikia kaya zaidi ya milioni moja zinazoishi katika hali ya umaskini.
Alisema utekelezaji wa kuziwezesha kaya maskini unahitaji
uwekezaji mkubwa kwenye mifumo na kujenga uwezo katika ngazi zote.
“Tasaf imejikita katika uhaulishaji fedha kwa kaya maskini
wakiwemo wazee , wajawazito na wanafunzi ili waweze kupata huduma za elimu na
afya.Pia inatoa ajira kwenye kaya hizo hususan zeye watu wenye uwezo wa kufanya
kazi,” alisema.
Alisema mpango huo wa kunusuru kaya maskini katika
Halmashauri ya Mji wa Kibaha, unatarajia kufikia asilimia 70 ya kaya katika
mitaa yote ya halmashauri.
No comments:
Post a Comment