Wednesday, October 22, 2014

BRELA yatoa somo kwa wafanyabiashara mjini Songea

Msajili msaidizi wa wakala wa usajili biashara na leseni (BRELA), Seka Kasera (kulia) akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara katika manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, muda mfupi mara baada ya kumalizika kwa zoezi  la kusajili  majina ya biashara zao ili kuweza kuzirasimisha na kutambuliwa na taasisi mbalimbali za fedha, zoezi la usajili wa biashara katika manispaa hiyo limefanywa na Wakala wa usajili wa biashara na leseni (BRELA), ikiwa ni hatua ya kuhamasisha wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda  kusajili biashara zao kwa wingi.
Msajili msaidizi wa wakala wa usajili na leseni (BRELA) Bw. Seka Kisera( kushoto) akiteta jambo na Afisa mtendaji wa chama cha wenye viwanda biashara na kilimo (TCCIA) mkoani Ruvuma,  Bw. Stanley Moyo wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara wa manispaa ya Songea, semina iliyoambatana na zoezi la kurasimisha biashara zao, zoezi hilo lilifanyika jana katika manispaa hiyo jana.
Na Mwandishi Wetu, Songea
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni nchini (BRELA) imeendelea kuwasisitiza wafanyabiashara kujitokeza kusajili majina ya biashara zao ili ziweze kurasimishwa, jambo ambalo litasaidia serikali kuwatambua wafanya biashara waliopo katika mkoa husika.

Akizungumza  kwenye Semina ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara mjini hapa juu ya umuhimu wa kusajili majina ya biashara zao ili ziweze kutambulika rasmi, Msajili Msaidizi wa Brela, Bw. Seka Kasera amewaomba wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi na kusajili biashara zao.

“Ni muhimu kwa wafanyabiashara hawa kusajili ili kutoa wigo mpana kwa serikali kuweka mipango yake vizuri ikiwa ni pamoja na suala nzima la ukusanyaji wa kodi,”alisema Bwana Kasera.

Alisisitiza kuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia wafanyabiashara hao kuweza kupata mikopo kwa wepesi katika taasisi mbalimbali za kibenki ambazo zimekuwa hazina imani kwa kiasi kikubwa na watu ambao hawajasajili biashara zao.

“Napenda niwaambie kuwa brela inatoa njia nyepesi sana, baada ya kusajili biashara kwenda benki kuomba mkopo linakuwa jambo rahisi sana,”alisisitiza na kuwapongeza wafanyabiashara wa manispaa ya songea kwa kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo kusajili biashara zao.


Bwana Kasera alisema mafunzo ambayo Brela imekuwa ikiyatoa kwa wafanyabiashara yamewasidia sana kuwajengea uwezo na kutambua umuhimu wa kusajili majina biashara.

No comments: