Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Matumaini ya Tanzania kuzalisha zaidi umeme kwa kutumia
vyanzo vya maji sasa ni makubwa.
Vyanzo mbalimbali vya maji vimeshagunduliwa, kutathminiwa na
kukubalika katika ngazi ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bonde la Mto
Rufiji (RUBADA), Bw. Aloyce Masanja, ikiwa miradi hiyo itatekelezwa, itasaidia
kwa kiwango kikubwa juhudi za serikali kupata nishati rahisi na ya uhakika kwa
maendeleo ya taifa.
Miradi ambayo iko tayari kutekelezwa ni pamoja na Stiegler’s
Gorge (2100 MW); mradi wa Mpanga (165MW); mradi wa Mnyera (485MW) na mradi wa
Iringa (80MW).
“Kama miradi hii ikitekelezwa kwa haraka, itasaidia kwa
kiwango kikubwa kuchangia kupatikana kwa nishati inayohitajika sana kwa sasa
kwa maendeleo,” alisema jana Mkurugenzi huyo alipokuwa akiongea na waandishi wa
habari.
Kwa mujibu wa Bw. Masanja, Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni limeshatathmini miradi hiyo na
kuikubali.
Aliongeza kuwa wadau wa kimataifa wameonyesha utayari wa
kushirikiana na wale wa ndani katika utekelezaji wa miradi hiyo bila kuhitaji ushiriki
wowote wa kifedha kutoka serikalini.
“Hii ni fursa ambayo watanzania hatuna budi kuitumia,”
alisema.
Katikati wa mwaka 2012, RUBADA ilitiliana saini na kampuni ya
Odebrecht International ili kuendeleza mradi wa Stiegler’s Gorge.
Kampuni ya Odebrecht inasifika kwa uzoefu wake wa siku nyingi
katika ujenzi wa miradi mikubwa ya mabwawa ya umeme duniani. Kampuni hii imehusika na ujenzi wa mradi wa
pili kwa ukubwa duniani nchini Brazil unaozalisha MW 14,000.
Ukishakamilika, mradi huu utachukua kilomita za mraba 1200 za
hifadhi ya Selous yenye ukubwa wa kilomita za mraba 54,000.
Kwa mujibu wa wataalamu, Bonde lote la Rufiji lina uwezo wa
kuzalisha MW 4,000 za umeme.
Tanzania iko katika juhudi mbalimba za kuhakikisha inapata
vyanzo mbalimbali vya nishati ya umeme ambayo inachukuliwa kama kiungo muhimu
katika kuchochea maendeleo ya taifa na kufikia malengo yake na kuleta neema kwa
wananchi.
No comments:
Post a Comment