Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Baadhi ya wananchi wameelezea kusikitishwa kwao na mwenendo
wa uharibifu unaozidi kushika kasi katika miundombinu ya mradi wa mabasi
yaendayo haraka (BRT).
Wakiongea kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesema
uharibifu huo unaofanywa kwa makusudi ni uhujumu uchumi na haukubaliki.
“Hali hii haikubaliki…ni lazima serikali iingilie kati
kuhakikisha uharibifu huu unakomeshwa mara moja,” alisema Juma Mohamed eneo la
Magomeni Mapipa jana jijini Dar es Salaam.
Uharibifu huo kwa kiwango kikubwa unatokana na baadhi ya raia
wasio waaminifu kuiba vifaa mbalimbali katika eneo la mradi huo kabla hata
haujakabidhiwa rasmi.
Vifaa vinavyoibiwa na kuharibiwa ni pamoja na mifuniko ya
mashimo ya mifumo ya maji, alama za barabarani, pamoja na kuharibiwa kwa
kiwango kikubwa kwa nguzo katika maeneo ya vivuko ili kuiba nondo zake.
Vifaa hivi vinaibwa kwa nia ya kuviuza kama vyuma chakavu.
Mwananchi mwingine, Bi. Rose Nicodemus alisema vitendo hivyo
vinatia doa nchi nzima.
“Ni lazima tubadilike kama jamii,” alisema.
Mkandarasi mkuu wa mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia
ni kampuni ya Strabag International ya Ujerumani.
Awali mradi huo ulipangwa kukabidhiwa mwisho mwa mwaka huu
tayari kwa kuanza, lakini dalili ni kuwa hilo litachelewa kutokana uharibifu
unaoendelea kutokea.
Naye mwananchi mwingine, Dr. Cecilia Revocatus aliiita hali hiyo
kama ‘aibu kwa watanzania’ na kutoa wito kwa vyombo husika kuhakikisha mradi
huo unakuwa na mafanikio hapa nchini na mfano kwa nchi jirani.
Hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Said Mecky
Sadick aliwaambia waandishi wa habari kuhusiana na taa za barabarani 28
zilizokwishaibiwa katika maeneo ya mradi huo na mifuniko ya chuma ya mifumo ya
maji zaidi 10 iliyoibiwa.
“Tuliamua kupeleka mbele makabidhiano ya mradi huu baada ya
kugundua kuwa uharibifu mkubwa ulikuwa umefanyika katika barabara hii mpya,”
alisema.
No comments:
Post a Comment