Kaimu Mkurugenzi Msaidizi, Barabara Mijini na Vijijini toka
Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Hassan Matimbe (katikati) akikata utepe kuzindua
rasmi mtambo wa kutengenezea lami ya maji jijini Dar es Salaam mwishoni mwa
wiki. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa
Starpeco Limited, Mhandisi Gratian Nshekanabo na Mwenyekiti wa kampuni hiyo,
Bw. Prashant Patel (kulia). Mtambo huo
unamilikiwa na kuendeshwa na Starpeco Limited.
Mkurugenzi Mtendaji wa Starpeco Limited, Mhandisi Gratian
Nshekanabo akifafanua jambo kwa Kaimu Mkurugenzi Msaidizi, Barabara Mijini na
Vijijini toka Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Hassan Matimbe (kushoto) wakati wa
uzinduzi wa mtambo wa kutengenezea lami ya maji jijini Dar es Salaam mwishoni
mwa wiki. Kulia ni Mwenyekiti wa kampuni
hiyo, Bw. Prashant Patel. Mtambo huo unamilikiwa na kuendeshwa na Starpeco
Limited.
Na Mwandishi wetu, Dar es
Salaam
Kwa mara ya kwanza kabisa,
Tanzania imeanza kuzalisha lami ya maji.
Mtambo wa kuzalishia lami
hiyo unaomilikiwa na kampuni ya Starpeco Limited ulizinduliwa mwishoni mwa wiki
jijini Dar es Salaam.
Lami hiyo ambayo kwa
kitaalamu inajulikana kama Bitumen
emulsions inatumika san asana katika ujenzi wa barabara na kuziba viraka vya
barabara zilizo haribika.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Starpeco Limited, Mhandisi Gratian Nshekanabo aliwaambia waandishi wa habari
wakati wa uzinduzi huo kuwa upatikanaji rahisi na wa uhakika wa bidhaa hiyo
utasaidia kwa kiwango kikubwa sekta ya ujenzi nchini.
“Teknolojia hii
itabadilisha jinsi tunavyofanya kazi za ujenzi na ukarabati wa barabara zetu,”
alisema.
Mkurugenzi huyo alisema
kuwa kampuni hiyo inafuraha kwa kuweza kujenga na kumaliza mradi wa mtambo huo
kwa viwango vinavyotakiwa.
“Mtambo huu umefuata
viwango vya kimataifa,” alisema, na kuongeza kuwa una uwezo wa kuzalisha lita
10,000 za lami hiyo kwa saa.
Mtambo umetengenezwa
Ukraine lakini vifaa vyake vingine vimetoka Italia na Ufaransa.
Mhandisi Nshekanabo amesema
mtambo huo utatengeneza ajira za moja kwa moja 25 na 100 zisizo za moja kwa
moja.
Kwa upande wake, Kaimu
Mkurugenzi Msaidizi, Barabara Mijini na Vijijini toka Wizara ya Ujenzi,
Mhandisi Hassan Matimbe alitoa pongezi kwa kampuni hiyo kwa uamuzi wa kuanzisha
mtambo huo.
Afisa Masoko Mkuu wa kampuni hiyo, Bw.
Jones Mkoka alisema mtambo huo unaendana na nia ya Tanzania kubadili hali ya
uchumi kufikia uchumi wa kati.
“Maendeleo ya viwanda ni moja ya njia
za kufikia lengo hilo,” alisema.
Alifafanua kuwa kampuni hiyo imeamua
kuanza kutengeneza lami hiyo ya maji hapa nchini ili badala ya kuagiza nje ye
nchi.
Kampuni hiyo pia inatarajia
kuuza lami hiyo nje hasa katika nchi za Maziwa Makuu ambapo haizalishwi kwa
kiwango cha kutosha.
“Kwa kutumia lami hii,
serikali itaweza kuokoa gharama za ujenzi wa barabara,”alisema Afisa huyo.
Kwa mujibu wa wataalamu, lami hiyo ya maji ndio yenye unafuu zaidi
kulinganisha na lami aina nyingine na pia rafiki kwa mazingira.
No comments:
Post a Comment