Wednesday, October 8, 2014

BRELA yatoa siku 90 kwa makampuni kuwasilisha taarifa za mahesabu

Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Msajili wa Makampuni, Bw. Frank Kanyusi akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu siku 90 zilizotolewa kwa kampuni zinazofanya kazi Tanzania kuwasilisha kwa Msajili Wa Makampuni marejesho ya mwaka yakiambatana na mahesabu ya Kampuni yaliyokaguliwa na kupitishwa na Mkaguzi anayetambulika.  Muda huo uliotolewa umeanza jana hadi Januari 5, 2015.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umetangaza siku 90 kwa wamiliki na wakurugenzi wa makampuni kuwasilisha taarifa zao za mwaka za mahesabu ya kampuni zao zilizokaguliwa na muhasibu anayetambuliwa kisheria,  vinginevyo kampuni zao zitafutwa na wao chukuliwa hatua za kisheria.

Afisa Mtendaji Mkuu wa wakala huo na Msajili wa Makampuni, Bw. Frank Kanyusi aliwambia waandishi wa habari jiji Dar es Salaam jana kuwa wamiliki na wakurugenzi hao wa makampuni wanatakiwa kutumia siku hizo kuwasilisha taarifa zao za mwaka pamoja na  mahesabu ya kampuni ili wasiweze kukabiliwa na sheria.

“Agizo hili la siku 90 sawa na miezi mitatu linaanza Oktoba 6, 2014 na litafikia kikomo January 5, 2015,”alisema.

Alisema kampuni itakayoshindwa kutekeleza agizo hilo ndani ya kipindi hicho itafutiwa usajili na wamiliki na wakurugenzi wake watafikishwa mahakamani kwa kosa la kutotoa taarifa za kampuni zao kwa mujibu wa sheria ya makampuni.

Alisema kifungu namba 128 kifungu kidogo cha kwanza na kifungu namba 132 kifungu kidogo cha pili cha Sheria ya Makampuni Sura ya 212 vinalazimisha kampuni  zote nchini kuwasilisha kwa msajili wa makampuni taarifa zake za kila mwaka pamoja na mahesabu yaliyokaguliwa.

Pia sheria hiyo inasema ni kosa kwa kampuni kutowasilisha taarifa pamoja na mahesabu yake kwa msajili wa makapuni.


Aidha matawi ya makampuni ya kigeni yaliyoandikishwa nchini Tanzania pia yanapaswa kuwasilisha mahesabu ya kila mwaka, chini ya kifungu namba 438 kifungu kidogo cha kwanza cha Sheria hiyo.

No comments: