Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe,
Taaluma, Profesa Josephat Itika (kushoto) akifafanua jambo wakati wa kongamano
la watafiti waliokuwa wakijadili kuhusu kilimo cha mkataba mwishoni mwa wiki
jijini Dar es Salaam. Katikati ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe,
Utawala na Fedha, Prof. Faustin Kamuzora na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho,
Prof. Daniel Mkude.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa
Joseph Kuzilwa (kushoto) akifafanua jambo wakati wa kongamano la watafiti
waliokuwa wakijadili kuhusu kilimo cha mkataba mwishoni mwa wiki jijini Dar es
Salaam. Katikati ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Minnesota Marekani,
Profesa Mark Sellemare na kulia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Jiografia na
Jiolojia toka chuo kikuu cha Copenhagen, Denmark, Profesa Niels Fold.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali imeshauriwa kuharakisha kutunga sheria na
kanuni zitakazosaidia kuongoza Kilimo cha mkataba ili wakulima wadogo waweze
kunufaika zaidi kutokana na shughuli za Kilimo.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Joseph
Kuzilwa alitoa ushauri huo hivi karibuni jijini Dar es Salaam katika warsha
iliyokuwa ikijadili matokeo ya mradi wa utafiti kuhusu kilimo cha mkataba
uliyofanywa na chuo hicho kwa kushirikiana na Chuo cha Mipango Dodoma na Chuo
Kikuu cha Copenhagen cha Denmark.
“Tunahitaji kuwa na sheria itakayolenga kuwasaidia
wakulima wadogo,”alisema.
Kilimo cha mkataba kinahusisha makubaliano kati ya
wakulima wakubwa na wakulima wadogo kwa kuwasaidia maarifa, teknolojia na
kununua mazao yao.
Alisema sheria hiyo inatakiwa kulenga kuleta suluhisho
kwa matatizo yanayowakumba wakulima wadogo ambao hawafaidiki vya kutosha hasa
katika mazao ya pamba, miwa na alizeti.
Akifafanua zaidi alisema kutokana na kutokuwepo kwa
sheria hiyo, mikataba kati ya wakulima hao na wakulima wakubwa wawekezaji
huwanyima fursa ya kuendelea.
“Tumefarijika kwamba serikali ipo mbioni kutunga
sheria mama ili kuona pande zote za Kilimo cha mkataba zinapata haki
inayostahili,” alisema.
Katika warsha hiyo watafiti waliwasilisha makala 25 za
tafiti juu ya Kilimo cha mkataba na kuonyesha faida na changamoto za Kilimo
hicho.
Ilikubaliwa katika warsha hiyo kuanzishwa kwa mtandao
wa watafiti kwa nchi za Afrika watakaokuwa wanashauriana na kubadilishana
uzoefu kuhusiana na maswala mbalimbali kuhusu kilimo cha mkataba.
No comments:
Post a Comment