Thursday, October 16, 2014

Dkt. Bilal ahimiza amani, upendo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Serikali imewataka viongozi wa dini zote nchini kuendelea kuliombea Taifa la Tanzania ili libakie na amani, utulivu na upendo miongoni mwa wananchi kwani ni tunu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DKT. Mohamed Gharib Bilal, ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kituo cha huduma cha Mwadhama Laurean Kadinali Rugambwa kilichopo katika kanisa la Mtakatifu Petro.

Amesema viongozi wa dini wanayo nafasi kubwa ya kuwafanya waumini wao kutambua umuhimu wa tunu iliyoletwa kwa wanadamu ili waweze kukabiliana na majukumu ya maisha yao.

“Viongozi wa dini mnayo nafasi kubwa ya kuwafanya waumini wenu kutambua umuhimu wa tunu hii,”alisema Dkt. Bilal hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Kituo hicho kimegharimu Tshs Bilioni Tatu.

Alisema mafanikio ya kukamilika kwa kituo cha Kadinali Rugambwa ni matokeo ya mshikamano na upendo uliojengeka ndani ya nchi ya Tanzania.

“Nawakumbusha watanzania wenzangu wote kuendeleza moyo huu wa kuchangia maendeleo yetu katika sekta mbalimbali,”alisema Makamu wa Rais.

Aliongeza kuwa kufunguliwa kwa kituo cha huduma cha Kadinali Rugambwa ni kielelezo tosha cha kukumbuka historia yake ya unyenyekevu uliotukuka kwani kiongozi huyo wa dini aliipenda Tanzania na watu wake na alihubiri amani ndani na nje ya Tanzania.

“Nawapongeza kwa kuchagua jina hili, Kadinali Rugambwa alikuwa kiongozi wa kipekee katika kueneza suala la amani kwa watanzania na hii ndio njia bora ya kuwaenzi viongozi hawa,”alisema.


Alisisitiza kuwa kuzinduliwa kwa kituo hicho katika siku ya tarehe 14.10.2014 siku ambayo Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere anatimiza miaka 15 tangu kufa kwake ni kielelezo tosha cha kuenzi amani, upendo na mshikamano miongoni mwa watanzania.

“Kama njia ya kumuenzi Mwalimu, tusiruhusu uvunjifu wa umoja wetu na kutugawa, serikali itaendelea kusimamia misingi ya waasisi wa Taifa letu,” alisisitiza.

No comments: