Na Mwandishi wetu, Geita
Baraza la Taifa la Biashara
(TNBC) linatarajia kuzindua baraza la biashara la Mkoa wa Simiyu hivi karibuni
na kufanya mikoa yote kuwa na mabaraza hayo yenye jukumu la kuhamasisha
uwekezaji na biashara katika mikoa husika.
Katibu Mtendaji wa Baraza
hilo, Bw. Raymond Mbilinyi amewaambia waandishi wa habari Mkoani Geita hivi
karibuni kuwa taratibu za kuzinduliwa kwa baraza katika mkoa huo zimefikia
pazuri.
“Tumebaki na mkoa mmoja wa
Simiyu katika kuhakikisha mabaraza yote nchini yanafanya kazi,”alisema wakati
wa uzinduzi wa baraza la biashara la mkoa wa Geita.
Alifafanua kuwa serikali
imejiwekea mkakati wa kuhakikisha mwaka 2025 nchi inafikia uchumi wa kati ambao
pia utawaletea maisha bora zaidi watanzania.
Alisistiza kuwa mabaraza ya
biashara ya mikoa yanawajibu wa kuwa kichocheo cha sekta binafsi kuimarika
zaidi na inachangia ukuaji wa uchumi.
Mabaraza ya biashara ya
mkoa yanaundwa na wadau toka sekta ya umma na binafsi na yanafanya kwa
kusimamiwa na TNBC.
Katibu Tawala wa Mkoa wa
Geita, Bw. Severine Kahitwa alihamasisha wawekezaji kwenda katika mikoa mipya
iliyoanzishwa.
Geita na Simiyu ni kati ya
mikoa mipya kuanzishwa na serikali Tanzania bara.
No comments:
Post a Comment