Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mkandarasi mkuu wa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo
haraka (BRT), Strabag International ametangaza mabadiliko ya matumizi katika
makutano ya barabara za Morogoro na Kawawa.
Mabadiliko hayo yanaanza leo tarehe 10 hadi tarehe 25 mwezi
huu.
Akitangaza mabadiliko hayo jana jijini Dar es Salaam, Afisa
uhusiano wa kampuni hiyo, Bw. Yahya Mkumba alisema mabadiliko hayo yanatokana
na matengenezo yatakayokuwa yanafanyika eneo hilo.
Akielezea zaidi, alisema magari yatakayokuwa yanatumia
barabara ya Kawawa kuelekea maeneo ya Kigogo na Msimbazi hayataweza kuendelea
moja kwa moja yatakapofika katika makutano hayo na badala yake yatalazimika
kuchepuka kushoto, katika barabara ya Morogoro na kutafuta njia mbadala.
Pia magari yatakayokuwa yanatokea eneo la kinondoni kwa
kutumia njia ya Kawawa hayataweza kuelekea Ubungo yatakapofika katika taa za
kuongozea magari za Magomeni.
Aidha, magari yatakayokuwa yanatokea eneo la Jangwani kwa
kutumia barabara ya Morogoro hayataruhusiwa kuelekea Kinondoni yatakapofika
katika makutano ya barabara hizo.
“Wananchi watuvumilie katika kipindi hiki na tunaomba radhi
kwa usumbufu wowote utakaotokea,” alisema.
Mradi wa BRT unalenga kupunguza msongamano wa magari jijini
Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment