Na Mwandishi wetu, Geita
Baraza la Biashara la Mkoa wa Geita limetakiwa kuongeza
ubunifu ili kuhakikisha mkoa huo unapiga hatua katika nyanja za uwekezaji na biashara
ili kuchangia ukuaji wa uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Bw. Said Magalula amesema mwishoni
mwa wiki akizindua rasmi baraza hilo kuwa wakati umefika kuhakikisha mkoa
unakuza uwekezaji na biashara.
“Baraza litumike kukuza biashara katika mkoa wetu
ambao una fursa nyingi za uwekezaji,”alisema Bw. Magalula ambaye pia ni mkuu wa
mkoa huo.
Mabaraza ya biashara ya mkoa yanaundwa na wadau toka
sekta ya umma na binafsi na yanafanya kazi chini ya Baraza la Taifa la Biashara
(TNBC).
Alisema kimsingi sekta binafsi ni injini ya maendeleo
na inasaidia kukuza uchumi na jambo kubwa ni kwa baraza kufanya kazi kwa bidii
na kwa ushirikiano.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, mkoa wa Geita una fursa
nyingi na unahitaji wawekezaji katika sekta za madini na viwanda vya kuongeza
thamani mazao ya mifugo, Kilimo miongoni mwa nyingine.
Alisema pamoja na kwamba mkoa huo una vikwazo vya biashara,
ni wajibu wa baraza hilo kujadili na kutoa mapendekezo ili serikali iweze kutafuta
ufumbuzi.
No comments:
Post a Comment