Meneja Msaidizi wa Lions
Clubs International, Bw. Benjamin Futransky (kulia) akiwa na Mratibu mkuu wa
surua-rubella wa klabu hiyo nchini, Bw. Abdul Majeed Khan wakati wa moja ya
shughuli za kuhamasisha wananchi kujitokeza kupata chanjo ya magonjwa hayo hivi
karibuni jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Klabu ya Lions International na wadau wengine wanatarajia
kukusanya jumla ya dola milioni 60 za Marekani ifikapo mwaka 2017 ili kuimarisha
kampeni ya chanjo ya surua na rubella barani Afrika, Tanzania ikiwa moja ya
nchi zitakazofaidika.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni jijini
Dar es Salaam, Meneja Msaidizi wa kablu hiyo, Bw. Benjamin Futransky alisema
fedha hizo zitapatikana kutoka kwa wanachama zaidi ya milioni moja waliopo
duniani kote kwa madhumuni ya kutoa huduma za afya hasa chanjo hiyo.
“Ni matarijio yetu kwamba fedha hizi zitapatikana na
kwamba zitatumika katika kuimarisha kampeni hii,” alisema.
Kampeni ya surua-rubella hufanyika hapa nchini kila baada
ya miaka mitatu.
Katika kampeni ya mwaka huu klabu ya Lions imetoa msaada
wa Dola za kimarekani milioni 12 (sawa na Tshs 20 bilioni) ili kufanikisha
zoezi hilo. Kampeni ya mwaka huu ilizinduliwa tarehe 18 mwezi huu na kilele
chake kitafikiwa leo tarehe 24 mwezi huu.
Kwa mujibu wa Meneja huyo, fedha hizo zitapatikana kwa
ushirikiano wa Klabu ya Lions International na Gavi Alliance ambapo zaidi ya
dola milioni 60 za Marekani zitakusanywa kwa lengo la kuendeleza kampeni ya
chanjo ya surua-rubella katika nchini mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania.
Akizungumzia maendeleo ya kampeni inayoendelea, alisema anaridhishwa
na mwitikio wa watu katika kuwapeleka watoto kupata chanjo na akatoa wito kwa
wananchi kuzidi kufika katika vituo vya tiba ili wapate chanjo.
No comments:
Post a Comment