Na Mwandishi wetu, Dar es salaam
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
imepandisha gharama za huduma hospitalini hapo na sasa mgonjwa atakayelazwa
atalazimika kulipia Sh.5000 kwa siku.
Gharama hizo zitalipwa kwa wagonjwa
wote wa rufaa, ilisema taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi mtendaji wa hospitali
hiyo,Dk. Marina Njelekela na kusambazwa kwenye vyombo vya habari.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa gharama
mpya zilianza kutumika Oktoba 17, mwaka huu. Hata hivyo, taarifa hiyo haikufafanua
uamuzi wa kupandisha gharama hizo.
Alipofuatwa ili kutolea ufafanuzi
mabadiliko hayo, Ofisa Uhusiano wa MNH, Aminiel Algaesh hakuwa tayari kusema
lolote , huku Dk. Njelekela naye akishindwa kupatikana.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Dk Steven Kebwe alisema hafamu lolote juu ya ongezeko la bei hizo.
“Sifahamu kuwapo na mabadiliko ya bei
za matibabu, ninachojua mimi gharama bado ziko chini,”alisema Kebwe.
Muuguzi wa hostipitali hiyo ambaye
hakutaka jina lake litajwe alisema gharama hizo zinahusisha malipo ya malazi ya
shilingi 5000 kwa siku na chakula shilingi 2000 kwa mlo mmoja, gharama ambazo
anasema hazikuwapo siku za nyuma.
Awali, wagonjwa walikuwa wanalipa
gharama za matibabu tu, huduma nyingine za malazi na chakula zilitolewa bure. Mabadiliko
hayo sasa yatamlazimu mgonjwa aliyepewa rufaa kulipia gharama hizo bila kujali
alikotoka.
Muuguzi huyo alisema idadi ya
wagonjwa imepungua wodini kutokana na wengi wao kushindwa kumudu gharama.
Amesema tangu utaratibu huo uanze,
kumekuwa na tofauti kubwa na zamani kwasababu wagonjwa ambao hawana uwezo wa
kulipia kiasi hicho, hawalali hospitali hata kama hali zao zingewataka kulazwa.
No comments:
Post a Comment