Afisa
Mifumo wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Fransis Mwakalebela
(kushoto) akitoa maelezo kwa baadhi ya wafanyabiashara wa manispaa ya Songea
mkoani Ruvuma mwishoni mwa wiki wakati wa zoezi la kusajili majina ya biashara
zao ili ziweze kurasimishwa na kutambulika. Zoezi hilo limefanyika kwa
siku tatu katika manispaa hiyo.
Na Mwandishi Wetu, Songea
Wafanyabiashara katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma
wamejitokeza kwa wingi katika zoezi la usajili wa majina ya biashara zao na kuielezea fursa hiyo kuwa mkombozi kwao.
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) uko mkoani
Ruvuma ukiendesha elimu kuhusu kazi zao pamoja na kutoa fursa kwa wakazi wa
mkoa huo kusajili jina la biashara kwa kutumia mfumo mpya wa kielektroniki
ulioanza kutumiwa na wakala hivi karibuni.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara Emmanuel
Kondoe, Deogratius Banda na Tatu Songambele wameonekana kuguswa na zoezi hilo
na kulielezea kuwa ni moja ya kichocheo kikubwa katika kuendeleza na kuimarisha
biashara zao.
“Suala la kusajili jina la biashara ni jambo la msingi ambalo
linatusaidia sisi wafanyabiashara wadogo na wa kati katika kuendeleza na kukuza
mitaji,” alisema Kondoe.
Aliongeza kuwa walikuwa wanatumia muda mwingi kwenda Dar es
Salaam kusajili jina, jambo ambalo lilikua linawagharimu muda pamoja na fedha
nyingi.
“Nimesajili jina kwa shilingi elfu sita tu, ningeenda Dar es
Salaam ningetumia zaidi ya laki 2 kwa usafiri, kula pamoja na kulala,”
aliongeza Kondoe.
Tatu Songambele aliielezea hatua ya BRELA kutembelea
wafanyabiashara mikoani ya kibunifu na mkombozi kwa wafanyabiashara wadogo.
“Wamefanya jambo kubwa sana kwetu wana Ruvuma…nimefurahishwa
nao,” alisema Bi. Songambele.
No comments:
Post a Comment