Friday, October 3, 2014

Watafiti: Kilimo cha mkataba ni mkombozi

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Joseph Kuzilwa (katikati) akifafanua jambo wakati wa kongamano la watafiti waliokuwa wakijadili kuhusu kilimo cha mkataba jana jijini Dar es Salaam.  Kulia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Minnesota Marekani , Profesa Mark Sellemare na kushoto ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Jiografia na Jiolojia toka chuo kikuu cha Copenhagen, Denmark, Profesa Niels Fold.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Watafiti wa ndani na nje wametaka kilimo cha mkataba kikuzwe Tanzania kwa kuwa kina nafasi kubwa ya kumuendeleza mkulima mdogo na kuleta maendeleo.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Joseph Kuzilwa alisema hayo jijini Dar es Salaam katika warsha iliyokuwa ikijadili matokeo ya mradi wa utafiti uliyofanywa na chuo hicho kwa kushirikiana na Chuo cha Mipango 
Dodoma na Chuo Kikuu cha Copenhagen cha Denmark.

Amewashauri wakulima wadogo nchini kuunda umoja kwenye vikundi vyenye nguvu ili waweze kuingia katika Kilimo cha mkataba kitakachowasaidia kupata maarifa zaidi ya kuendesha shughuli za  Kilimo hapa nchini na kuchangia maendeleo.

“Wakulima wadogo nchini wanatakiwa kuwa na  umoja wao na vikundi ambavyo vitawawezesha kuingia katika mfumo wa Kilimo cha mkataba,” alisema Prof. Kuzilwa.

Kilimo cha mkataba kinahusisha wakulima wakubwa kuingia makubaliano na wakulima wadogo kwa kuwasaidia maarifa, teknolojia na hata kununua mazao yao.

Alifafanua kuwa kilimo cha Tanzania kinaweza kuimarika zaidi ya hapa kilipo, kama wakulima wadogo wataanza kutengeneza umoja wenye vikundi vyenye nguvu na kuingia katika Kilimo cha mkataba.


Warsha hiyo ilifunguliwa Alhamis wiki hii na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Profesa Daniel Mkude.

No comments: