Tuesday, September 30, 2014

Mzumbe mwenyeji wa kongamano la kimataifa la kilimo cha mkataba

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Wataalamu mbalimbali toka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kukutana jijini Dar es Salaam leo katika kongamano la siku mbili litakalozungumzia kilimo cha mkataba Afrika.

Kongamano hilo limetayarishwa na Chuo Kikuu Mzumbe; Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini cha Dodoma na Idara ya Jiografia na Taasisi ya Chakula na Uchumi vya Chuo Kikuu cha Copenhagen kupitia mradi unaoangalia fursa na changamoto za kilimo cha mkataba.

Akitangaza mkutano huo jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Chuo Kikuu Mzumbe, Bi. Rainfrida Ngatunga alisema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya Chuo hicho na msomi aliyebobea, Prof. Daniel Mkude.

“Inatarajiwa kuwa kongamano hilo litasaidia katika kujenga mtandao wa kubadilishana maarifa na uzoefu kuhusiana na kilimo cha mkataba na mabadiliko ya maeneo ya vijijini Afrika,” alisema.

Baadhi ya mada zitakazojadiliwa ni pamoja na maswala mapya yanayojitokeza kuhusu kilimo cha mkataba na sera, ufanisi katika uzalishaji, kilimo cha mkataba, mapato na faida na uzoefu wa kimahtaifa.

Mada zitakazotolewa zitachapishwa katika jarida maalumu la kimataifa.

Kongamano hilo litamalizika kwa kufanyika kwa mkutano wa majadiliano ambapo washiriki watapendekeza sera na mambo muhimu yatakayotakiwa kushughulikiwa na watunga sera.

Kongamano hilo limewezeshwa na msaada wa utafiti kwa Chuo Kikuu Mzumbe toka serikali ya Denmark kupitia Danish Fellowship Centre.


Mwisho

No comments: