Monday, September 29, 2014

Wasimamizi miradi sekta ya maji watakiwa kuongeza juhudi, umakini

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Serikali imewataka watekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta ya maji kuzipa kipaumbele kazi za usimamizi ili zikamilike ndani ya muda uliopangwa kwa mujibu wa mikataba.
 
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe amesema hilo likifanyika vyema litasaidia kupatikana mafanikio katika kufikia malengo ya Awamu ya Pili ya Utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.
 
Alikuwa akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa awamu hiyo ya pili ambayo imeanza kutekelezwa tarehe 1 Julai 2014 hadi tarehe 30 Juni 2019.
 
“Hii itasaidia kwa kiwango kikubwa kufikiwa kwa malengo tuliyojiwekea,” alisema.
 
Awamu ya Kwanza ya Programu hiyo ilianza kutekelezwa Julai mosi 2007 na kukamilika tarehe 30 Juni 2014.
 
Waziri Maghembe pia aliwaagiza watekelezaji hao wa miradi kuhakikisha kuwa utekelezaji wa miradi hiyo wanayoisimamia inalingana na viwango vya kitaalam.

“Wakati huo huo mzingatie viwango vya uaminifu ambavyo huonekana kwa macho ya kila mtu siyo wahandisi pekee ambao huona kuwa baadhi ya miradi huwa hailingani na thamani ya fedha iliyotumika,” alisema.
 
Waziri Maghembe aliwashukuru washirika wa maendeleo kwa ushirikiano waliouonyesha wakati wa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Programu.
 
“Naomba wadau wote tuendelee kushirikiana katika utekelezaji wa awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji tunayoizindua leo,” alisema.
 
Jumla ya fedha zinazohitajika kutekeleza awamu ya pili ya programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ni Dola za Marekani Trilioni 3.34. 
 
Waziri alisema fedha zitatokana na Bajeti ya Serikali ambayo pia itachangiwa na Washirika wa Maendeleo.
 
“Pia nategemea ushiriki mkubwa wa sekta binafsi kwenye uwekezaji hasa kwenye miradi ya maji mijini,” aliongeza.
 
Alisema ili kufikia malengo katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa Awamu hiyo ya Pili mafunzo na uzoefu uliopatikana wakati wa kutekeleza awamu ya kwanza ya Programu utatumika vyema.
 
“Tunahitaji kuongeza ushirikiano zaidi baina yetu sisi wenyewe kama watanzania, na pia kuongeza wigo wa ushirikiano wetu na Washirika Wetu wa Maendeleo,” alisema. 
 
Aliwaomba washirika wa Maendeleo waongeze ushiriki wao kwenye sekta ya maji kwa sababu serikali imeamua kwa dhati kuongeza kasi ya utekelezaji na viwango vya ufuatiliaji na usimamizi wa miradi. 
 
Alisema ni imani yake kwamba kila mmoja akitimiza wajibu wake, kupitia Programu hii, malengo yaliyokubalika yatafikiwa; hususan kusimamia vizuri uendelezaji wa rasilimali za maji, kuwapatia wananchi huduma bora za maji safi na salama, pamoja na kuboresha huduma za usafi wa mazingira.
 
Madhumuni makuu ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ni kuhakikisha kuwa Sekta ya Maji inayafikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ifikapo mwaka 2025; yenye dhima ya kuwapatia wakazi wote wa mijini huduma za maji safi na salama na kuwapatia huduma hizo angalau asilimia 90 ya wakazi wa vijijini.
 
Mwisho 

No comments: