Monday, September 15, 2014

TNBC yawataka watendaji Njombe kutumia vyema baraza la biashara la mkoa

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, kapteni Mstaafu Asei Msangi akifurahia jambo na Mkurugenzi wa Biashara wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC), Bw. Arthur Mtafya (kulia) na Mwenyekiti wa TCCIA mkoa wa Njombe  Bw. Mhema Oraph (Katikati) wakati wa uzinduzi wa baraza la biashara la mkoa huo hivi karibuni mkoani Njombe.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, kapteni Mstaafu Asei Msangi (kushoto) akiwa pamoja na Mkurugenzi wa Biashara wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC), Bw. Arthur Mtafya wakati wa uzinduzi wa baraza la biashara la mkoa huo hivi karibuni mkoani Njombe.
Na Mwandishi wetu, Njombe

Watendaji wa wilaya za mkoa wa Njombe wametakiwa kutumia fursa ya uwepo wa Baraza la Biashara la Mkoa kuunganisha sekta ya umma na binafsi kujadili kutatua changamoto zilizopo katika biashara na kutumia fursa hiyo katika kutangaza vivutio vya biashara zilivyopo katika mkoa huo. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa baraza hilo, Mkurugenzi wa Biashara wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC), Bw. Arthur Mtafya alisema wajumbe wa baraza hilo la mkoa hawana budi ku kuzingatia fursa za uchumi zilizo katika mkoa huo na kujadiliana juu ya vikwazo vya biashara ili kupanua wigo wa uwekezaji mkoani humo.

“Nia ya kuanzisha baraza katika ngazi ya mkoa na wilaya ni kurahisisha utendaji kutoka ngazi ya taifa mpaka wilayani kwani kuna mambo yanayoweza kushughulikiwa katika ngazi ya mkoa,” alisema hivi karibuni mkoani humo. 

Bw. Mtafya alisema sera za nchi zinaruhusu baadhi ya changamoto zinazohusu mkoa fulani zitatuliwe katika ngazi ya mkoa na kwamba hiyo inasaidia utendaji na uwajibikaji na kuwa yanaposhindikana ndipo huwasilishwa katika ngazi ya taifa ili kufanyiwa kazi.

Alisema ushiriki kamilifu wa sekta hizo mbili katika ngazi ya mkoa na wilaya utasaidia kwa kiwango kikubwa katika kuinua hali ya biashara na uwekezaji katika mkoa huo wa Njombe.

“Msifanye kazi kwa matukio au mazoea bali pawepo na muundo maalum wa kazi na mgawanyo wa majukumu na muda maalum wa kuwasilisha kazi na kuzitafutia ufumbuzi,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe, kapteni Mstaafu Asei Msangi alisema baraza hilo jipya litakuwa chachu ya maendeleo kwa kuunganisha sekta ya umma na binafsi katika kujadili vikwazo vya biashara ili kukuza uchumi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.

“Tutumie fursa hii kutangaza vivutio vya biashara vilivyopo mkoa wa Njombe ili kupata wawekezaji katika maeneo tofauti,” alisema.

Vivutio vilivyopo katika mkoa huo ni pamoja na Uvuvi, Utalii, kilimo, makaa ya mawe na mbao.
 
Katika mkutano huo, ziliundwa kamati saba kulingana na vivutio vilivyopo katika mkoa huo ili kurahisisha utendaji wa baraza hilo.
 
Kamati zilizoundwa ni Kilimo na Chakula, Ufugaji na Uvuvi, Nishati na Madini, Ardhi na Maliasili, Mazingira na Utalii, Viwanda na Biashara pamoja na kamati ya Huduma za jamii.
 
Naye mwenyekiti wa TCCIA mkoa wa Njombe  Bw. Mhema Oraph alisema uwepo wa baraza hilo ni mwanzo mzuri wa kuimarisha maendeleo katika mkoa huo. 
 
Aliwataka wadau wa baraza hilo kuhakikisha kuwa wanashirikiana kwa karibu ili kutekeleza maswala watakayokubaliana kwa urahisi na ufanisi.
 
Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau kutoka sekta ya umma na binafsi pamoja na makatibu tawala wa wilaya zilizopo mkoani Njombe miongoni mwa wengine.
 
Mwisho
 

 


No comments: