Tuesday, September 9, 2014

Wananchi watakiwa kuacha kuhifadhi fedha majumbani

Mwanasheria wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB), Bw. Rashid Mrutu akielezea jambo kuhusiana na kazi zinazofanywa na chombo hicho wakati wa maonyesho ya Wiki ya Huduma za Kifedha na Uwekezaji yaliyomalizika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Bodi ya Bima ya Amana imewataka wananchi kujenga utamaduni na kuendelea kuweka pesa benki kwani ni njia salama na faida zake kiuchumi kwao na kwa nchi ni kubwa.

Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mwanasheria wa Bodi hiyo, Bw. Rashid Mrutu alisema utamaduni wa kuweka pesa benki unajenga mahusiano na mabenki hivyo kujitengenezea nafasi ya kupata mikopo.

Afisa huyo alisema amana zinazowekwa na wateja wa benki zinatoa fursa kwa vyombo hivyo vya fedha kukopesha makampuni na wafanyabiashara, na hivyo kuendesha uchumi.

“Wananchi waache mtindo wa kuficha fedha kwenye magodoro…hii ni hatari kwao,” alisema wakati wa maonyesho ya Wiki ya Huduma za Kifedha na Uwekezaji yaliyomalizika mwishoni mwa wiki.

Bodi hiyo ilishiriki katika maonyesho hayo kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na huduma inazotoa.

Aliwatoa wasiwasi wananchi kuhusiana na usalama wa fedha zao akisema kuwa nia ya bodi hiyo ni kuhakikisha kuwa inalinda kwa mujibu wa sheria amana zao na kuwalipa iwapo lolote litatokea kama kufilisika kwa benki.

Akielezea majukumu ya bodi hiyo, alisema ina jukumu la kukusanya michango kutoka kwenye taasisi za fedha na benki ambazo zimepewa leseni na benki kuu.

“Hao ni wanachama wanochangia katika mfuko wa bodi ya bima ya amana, ambao unasaidia kulipa wateja wa mabenki pale benki inapofilisika,” alisema.

Pia alisema bodi hiyo huwekeza fedha zinazokusanywa kama michango kutoka kwa benki na taasisi za fedha na kulipa wateja wa mabenki pale ambapo benki inapofilisika.

“Pia tunasimamia ufilisi wa benki au taasisi ya fedha pale ambapo inafilisika na bodi hii imeteuliwa na benki kuu kufanya hiyo kazi,” alieleza.

Akielezea zaidi, Bw. Mrutu alisema tangu kuanzishwa kwa bodi hiyo, wamekuwa wakiangalia kila wakati kiwango cha bima wanachotakiwa kulipa iwapo patatokea matatizo ya kufilisika kwa benki.

Bodi ya Bima ya Amana ilianzishwa mwaka 1994 ikiwa na dhumuni la kuwa na chombo ambacho kitatoa bima ya amana, ambapo wale wenye bima ya amana watapata fidia endapo benki itafilisika.

Chombo hicho kinachangiwa na benki na taasisi yeyote ya fedha ambayo imepewa leseni na Benki kuu ya Tanzania na kwa mujibu wa sheria taasisi hizo zinatakiwa kuwa wanachama wa bodi hiyo.

Mwisho



No comments: