Na Mwandishi
wetu, Dar es Salaam
Wakazi wa Mbeya
na vitongoji vyake wamehamasishwa kujitokeza kwa wingi kufahamu kazi za Wakala
wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) katika wiki ya uhamasishaji itakayoendeshwa
na wakala huo kuanzia leo.
Akitangaza
tukio hilo la uhamasishaji kwa waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar
es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA na Msajili wa Makampuni, Bw. Frank
Kanyusi Frank alisema wameamua kufanya hivyo kwa kuwa wananchi wengi hawafahamu
kazi za wakala na jinsi wanavyoweza kufaidika.
“Tumegundua
watu wengi hawafahamu BRELA inafanya nini hasa na jinsi gani wanaweza kufaidika
na wakala huu,” alisema.
Alisema hii ni
nafasi muhimu kwa wakazi wa Mbeya na vitongoji vyake na hivyo kuwataka
kujitokeza kwa wingi kufaidika na elimu watakayokuwa wanatoa.
“Tumeanza na
Mbeya…mikoa mingine itafuata,” alisema.
Pamoja na elimu
hiyo, pia wakazi wa Mbeya watafaidika na usajili wa papo kwa hapo wa jina la
biashara utakaokuwa unafanywa na BRELA kwa kutumia mfumo mpya wa kielektroniki
ulioanza kutumiwa na wakala hivi karibuni.
“Wakazi wa
Mbeya watumie nafasi hii pia kusajili majina ya biashara papo kwa hapo kwa
kutumia teknolojia ya kisasa kabisa,” alisema.
Wataalamu wa
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa BRELA wamebuni mfumo ambao
utawawezesha watu kusajili jina la biashara kwa urahisi na ufanisi zaidi kuliko
ilivyokuwa ikifanyika hapo nyuma.
Kwa mujibu wa
afisa huyo mfumo huo uliobuniwa mwezi wa Sita mwaka huu umeonyesha kuwa na
ufanisi mkubwa na wa manufaa.
“Watu
wanaosajili jina la biashara wameongezeka mara dufu na malalamiko yamepungua
kwa kiwango kikubwa,” alisema.
Akizungumzia
faida za mfumo huo mpya, alisema utawawezesha watu wengi zaidi kuwa na majina
rasmi ya biashara na hivyo kufahamika zaidi na vyombo vya fedha na kuweza
kupata mikopo.
Pia alisema
mfumo huo utaiwezesha serikali kufahamu watu waliosajiliwa kisheria na hivyo
kurahisisha swala zima la ukusanyaji kodi.
Wiki hiyo ya
uhamasishaji inaendeshwa hadi tarehe 29 mwezi huu.
Urahisi wa
usajili wa jina la biashara ni kiashiria muhimu wa mazingira ya biashara katika
nchini.
Tanzania
inafanya juhudi kubwa kuhakikisha kuwa inaimarisha mazingira yake ya kufanya
biashara ili kuvutia zaidi wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment