Thursday, September 11, 2014

BRELA yarahisisha usajili wa jina la biashara kwa masaa 8 tu

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umetangaza kupunguzwa kwa muda wausajili wa jina la biashara kwa kiwango kikubwa.

Sasa usajili wa jina la biashara utachukua muda wa saa nane tu za kazi badala ya zaidi ya siku saba zilizokuwa zikitumika kabla.

Akitangaza hatua hiyo jana jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA na Msajili wa Makampuni, Bw. Frank Kanyusi Frank alisema maendeleo hayo yanalenga miongoni mwa mambo mengine kuimarisha mazingira ya biashara nchini Tanzania.

“Sasa usajili wa jina la biashara utafanyika kwa mfumo wa elektoniki,” alisema.
Akielezea zaidi alisema wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wamebuni mfumo ambao utawawezesha watu kusajili jina la biashara kwa urahisi na ufanisi zaidi kuliko inavyofanyika sasa.

Kwa mujibu wa afisa huyo mfumo huo uliobuniwa mwezi wa Sita mwaka huu umeonyesha kuwa na ufanisi mkubwa na wa manufaa.

“Watu wanaosajili jina la biashara wameongezeka mara dufu na malalamiko yamepungua kwa kiwango kikubwa,” alisema.

Akizungumzia faida za mfumo huo mpya, alisema utawawezesha watu wengi zaidi kuwa na majina rasmi ya biashara na hivyo kufahamika zaidi na vyombo vya fedha na kuweza kupata mikopo.

Pia alisema mfumo huo utaiwezesha serikali kufahamu watu waliosajiliwa kisheria na hivyo kurahisisha swala zima la ukusanyaji kodi.     

Alisisitiza kuwa watu wasidanganywe na mtu yeyote kuhusiana na utaratibu wa kusajili jina la kampuni na kuwa hakuna mtu wa kati atakayehusika.
“Wananchi wasidanganywe na vishoka wanajifanya kuwapa msaada kwa hili,” alisema.

Akielezea utaratibu kwa kifupi alisema mtu anayeomba kusajili jina la biashara atatakiwa kujaza fomu maalumu, kukadiriwa malipo na kulipia benki kasha kurudisha fomu hiyo BRELA ambapo taratibu nyingine zote zitashughulikiwa kielektroniki.

Urahisi wa usajili wa jina la biashara ni kiashiria muhimu wa mazingira ya biashara katika nchini.
Tanzania inafanya juhudi kubwa kuhakikisha kuwa inaimarisha mazingira yake ya kufanya biashara ili kuvutia zaidi wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Mwisho


No comments: