Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Said Meck Sadick ( kushoto) na
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam,Bw. Ramadhan Madabida
(kulia) wakipewa maelezo ya hatua za utekelezaji wa Mradi wa Mabasi yaendayo
Haraka kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa DART,Bi. Asteria Mlambo
(katikati) wakati wa ziara ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM
Mkoa, walipofanya ziara na kukagua miundombinu ya mradi huo barabara ya
Morogoro jijini mwishoni mwa wiki. ( wa pili kutoka kulia) Meneja wa Mradi wa
kutoka Wakala wa Barabara nchini(TANROADS) mhandisi Barakaeli Mmari.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mradi wa Mabasi
yaendayo Haraka ( DART) Bi. Asteria Mlambo (kushoto) akitoa maelezo kwa
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam,Bi. Ramadhan Madabida (katikati)
wakati wa ziara ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho mkoa,
walitembelea na kukagua mradi wa mabasi yaendayo haraka barabara ya
Morogoro, ( kulia) ni Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick mwishoni
mwa wiki.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wajumbe wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
mkoa wa Dar es Salaam, wameelezea kuridhishwa na hatua kubwa iliyofikiwa katika
utekelezaji wa mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT).
Mradi huo uko chini ya wakala wa mradi wa mabasi yaendayo haraka
(DART).
Wajumbe hao walikuwa katika ziara ya kutembelea miradi
mbalimbali yamaendeleo inayotekelezwa na serikali katika mkoa huo hivi karibuni.
“Tumeridhishwa sana…mradi unaotekelezwa na DART ni mradi
uliotuvutia, tunawapongeza kwa juhudi kubwa,” alisema Mwenyekiti wa CCM, mkoa
wa Dar es Salaam, Bw. Ramadhani Madabida.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya
kutembelea mradi huo kutoka kivukoni hadi kimara, Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa
alisema hatua iliyofikiwa na DART ni kubwa na inahitaji kuungwa mkono na wadau
wote ili waweze kufanikiwa katika awamu
ya kwanza ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 80.
“Haya ndio mambo ambayo watanzania tunatakiwa kujivunia
kwa sababu miradi kama hii katika nchi zetu za kiafrika ni michache sana,”
alisema.
Alisisitiza kuwa miradi mikubwa kama ulivyo wa BRT inahitaji
utunzaji wa hali ya juu, ikiwa ni pamoja na nidhamu ya wananchi kuona kuwa
jambo lililofanyika ni kwa ajili yao na si mtu mwingine.
“Naomba niwaambie watanzania wenzangu hasa wana Dar es
Salaam, wakala umefanya kazi kubwa katika kusimamia mradi huu, kila mmoja awe
mlinzi wa mwenzake katika kulinda miundombinu hii,” alisisitiza Mwenyekiti
huyo.
Aliongeza kuwa utunzaji wa miundo mbinu unahitajika kwa
kila mwananchi katika eneo lote lililopitiwa na mradi jambo alilosema litasaidia
barabara hiyo kudumu kwa muda mrefu zaidi.
“Huu ni uwekezaji mkubwa sana na kioo cha jiji letu, mradi
huu utakapo kamilika jiji la Dar es Salaam litabadilika,” aliongeza.
Awali, akitoa maelezo mbele ya wajumbe hao, Mtendaji Mkuu
wa wakala wa DART, Bi. Asteria Mlambo alisema mradi unaendelea vizuri na uko
katika hatua za mwisho za utekelezaji wake.
“Mradi unakwenda vizuri na hatua iliyofikia sasa ni hatua
ya mwisho kwa sababu hadi sasa imebaki asilimia 20 ili uweze kukamilika,”
alisema.
Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano katika kuwabaini wale
wote wanoharibu miundo mbinu ya barabara hasa katika maeneo ya Manzese na Magomeni
kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi wanapoona hujuma inafanyika.
“Baadhi ya watu wasio waaminifu tayari wameanza kuiba
miundombiu iliyowekwa jambo ambalo si la kistaarabu na wanaofanya hivyo ni
vijana wetu wenyewe,” aliieleza kamati hiyo.
Aidha aliwataka wale wote wanaofanya biashara katika
maeneo ya mradi kuondoka mara moja kabla ya sheria hazijafuata, ili kutoa
nafasi kwa mkandarasi kufanya kazi zao pasipo usumbufu wowote.
Alisema Halmashauri ya Manispaa ya kinondoni inatakiwa
kuliangalia jambo hili kwani liko ndani ya uwezo wao ili watu wanaofanya biashara
ndani ya maeneo ya mradi kuondoka mara moja.
Mwisho
No comments:
Post a Comment